MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, amesema Tanzania imejitolea kikamilifu katika kuhifadhi, kutumia bahari na rasilimali zake kwa njia endelevu ili kufanikisha utekelezaji wa lengo namba 14 la maendeleo endelevu.
Dk. Mpango alisema hayo wakati akihutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhifadhi wa bahari na rasilimali zake unaofanyika jijini Lisbon, Ureno.
Amesema Tanzania imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kutenga sera, mikakati na mipango ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira ikiwemo kudhibiti mifuko ya plastiki.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imetunga sheria zinazoongoza usimamizi wa rasilimali za bahari na fukwe.
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, serikali imeendelea kufanya miradi inayohusiana na kusimamia, kulinda, kuhifadhi na kurejesha mifumo ikolojia ya bahari na kutenga asilimia 6.5 ya sehemu ya Bahari ya Hindi kuwa maeneo tengefu ya bahari, kudhibiti uvuvi haramu kwa asilimia 99 na kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za uvuvi wa bahari kuu.
Amesema Tanzania imejaliwa ukanda mrefu wa pwani wa takriban kilomita 1,450 na Ukanda wa Kiuchumi wa Kipekee unaofikia kilomita za mraba 223,000.
Dk. Mpango ametaja eneo la maji linalochukua kilomita za mraba 64,000, hivyo kuifanya nchi kuwa tajiri kwa bionuai na uwezo mkubwa wa uchumi wa bluu unaosaidia maisha ya mamilioni ya watu na usalama wa chakula na njia ya usafiri.
Ametoa wito kwa mataifa kuhakikisha unafanyika uwekezaji katika sayansi, uvumbuzi na ushirikiano wakati wa kutafuta suluhisho za changamoto zinazokabili bahari.
Dk. Mpango amesema kuna umuhimu wa kuunganisha nguvu na kuwekeza katika teknolojia za kibunifu za kupiga vita na kupambana na uvuvi haramu na kuhusisha jamii katika kuzuia uchafuzi wa bahari.
Makamu wa Rais amewakaribisha wawekezaji kushirikiana na Tanzania, hasa katika uhawilishaji wa teknolojia rafiki na sahihi, kujenga uwezo na utafiti ili kubuni njia endelevu za kukabiliana na changamoto zilizopo katika sekta ya bahari.
Dk. Mpango yupo nchini Ureno kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhifadhi wa Bahari na Rasilimali zake wenye lengo la kuhamasisha juhudi za mataifa katika kufanikisha utekelezaji wa lengo la 14 la maendeleo endelevu.
Na MWANDISHI MAALUMU, Ureno