RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amepongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China za kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu Zanzibar, katika mazungumzo kati yake na timu ya madaktari bingwa kutoka Jimbo la Jiangsu nchini China wanaotoa huduma katika hospitali za Zanzibar, baada ya kukabidhiwa na timu hiyo dawa na vifaatiba mbalimbali.
Alisema kwa kipindi kirefu serikali ya China imekuwa ikiisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya kwa kutoa vifaa, dawa na madaktari wanaokwenda kuhudumia visiwani humo.
Rais Dk. Mwinyi aliishukuru timu hiyo ya madaktari 21 kutoka China ambao wanatoa huduma za afya nchini hivi sasa na kubainisha misaada hiyo kwa kiasi kikubwa itapunguza uhaba wa madaktari bingwa, dawa na vifaatiba katika hospitali za Zanzibar.
Aliipongeza timu hiyo kwa kutoa huduma za afya zikiwemo za upasuaji wa kutumia teknolojia ya kisasa ambazo zimeimarisha sekta ya afya nchini.
Dk. Mwinyi alieleza kufarijika na juhudi zinazochukuliwa na timu hiyo ya kusomesha madaktari wazalendo wanaotoa huduma za afya katika hospitali kadhaa za Unguja na Pemba.
Pia, alieleza hatua zinazoendelea kuchukuliwa na SMZ za kuweka mazingira mazuri katika kuimarisha sekta ya afya na ujenzi wa hospitali za wilaya zitaimarisha zaidi huduma kwa upande wa Unguja na Pemba.
Naye, Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui, alisema wizara na timu hiyo ya madaktari wana ushirikiano mkubwa huku akieleza dawa na vifaatiba hivyo vinagharimu zaidi ya sh. milioni 300.
Kiongozi wa timu hiyo kutoka China, Dk. Qu Li Shuai alimueleza Dk. Mwinyi juhudi zinazochukuliwa na madaktari 21 ambao kati ya hao 12 wanatoa huduma katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na tisa Hospitali ya Abdalla Mzee Kisiwani Pemba.
Akitoa ufafanuzi juu ya misaada hiyo, Song Jianqing alisema msaada huo ni mwendelezo wa utamaduni wa uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na China uliowekwa na waasisi wa nchi hizo.
Jianqing alisema timu hiyo iliwasili Zanzibar Septemba, mwaka jana na imeanza kufanya kazi vizuri na tayari imetibu zaidi ya wananchi 50,000 na kuwafanyia upasuaji wagonjwa 6,000 katika hospitali za Mnazi Mmoja, Abdalla Mzee na Kivunge.
Alieleza katika kuendeleza uhusiano na ushirikiano huo wa kihistoria uliopo, timu ya madaktari bingwa wameanzisha mafunzo kwa madaktari wazalendo hatua ambayo itazidi kuimarisha sekta ya afya Zanzibar.
Aidha, alieleza jinsi walivyofanya upasuaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa Zanzibar ambayo ya kwanza kufanyika katika hospitali za Tanzania.
Alisema tayari wamefanya upasuaji za koo, masikio, macho, uchunguzi wa mfumo wa njia ya chakula ambao mwanzo huduma hizo zilikuwa zikipatikana Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa Jianqing, miongoni mwa vifaa walivyosaidia ni ECG defibrillator, potable echocardiography machines, probes, trocar kwa ajili ya upasuaji wa laparoscopic, video yalaryngoscope, electric negative pressure suction devices, oxygen generators, multifunctional monitors, mesh, surgical sutures na vinginevyo.
Na MWANDISHI MAALUMU

(Kulia kwa Dr Qu ) Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui.
