Na Mwandishi Wetu
NAIBU Spika, Dk. Tulia Ackson, amewataka wadau na taasisi za kifedha kujitokeza ili kuzisaidia kata ambazo hazina shule za sekondari kama vile za Izawa na ya Itagano za jijini Mbeya.
Aliyasema hayo jana, alipokuwa mgeni rasmi wakati wa makabidhiano ya mabati 324, yaliyotolewa na Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB), kwa ajili ya kusaidia kuezeka vyumba sita vya madarasa ya Shule ya Sekondari Itende, iliyoko Kata ya Itende, Mbeya, ambayo haina shule ya sekondari.
Alisema mchango huo unaunga mkono jitihada za Rais Dk. John Magufuli, kuendeleza kujenga na kukarabati miundombinu ya elimu ili kuendelea kuboresha elimu inayotolewa na kutoa maarifa na ujuzi wa kutosha kwa wahitimu.
Dk. Tulia, aliishukuru benki hiyo kwa kusaidia kata ya Itende, ambayo haina shule ya sekondari, jambo ambalo linawalazimu watoto kwenda mbali ili kuitafuta elimu hiyo.
Naibu Spika Dk. Tulia, aliwaomba wadau na benki kujitokeza ili kuzisaidia kata nyingine, ambazo nazo hazina shule za sekondari kama vile kata ya Izawa na kata ya Itagano, zote kutoka jiji la Mbeya.
“Naomba nitumie fursa hii kutoa wito kwa taasisi nyingine za kifedha, kuunga mkono jitihada za serikali za kuendelea kuboresha sekta ya elimu nchini,” alisema.
Kwa mujibu wa Naibu Spika, shule hiyo inategemea kuanza mwaka 2022, kwa kidato cha kwanza.
Awali, akikabidhi msaada huo, Mkurugenzi wa Mipango, Mikakati na Mahusiano ya Kitaasisi wa TIB, Patrick Mongella, alisema benki hiyo imekabidhi msaada huo kwa kutambua nafasi yake kama taasisi ya maendeleo, ili kuongeza ustawi wa sekta ya elimu katika Manispaa ya Jiji la Mbeya na Taifa kwa ujumla.
“Kwa kutambua ukweli kuwa suala la elimu ni mojawapo ya maeneo tunayoyaunga mkono, tuliona ni vema taasisi yetu itoe mchango kwa kuisaidia Manispaa ya Jiji la Mbeya, kukamilisha miundombinu ya elimu kwa wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza,” alisema.
Alisema anaamini msaada huo utachangia malengo ya serikali ya kuendelea kuboresha elimu inayotolewa ili itoe maarifa na ujuzi wa kutosha kwa wahitimu katika nyanja zote za elimu hapa nchini.