Duals, Milioni saba zamng’oa Papii Kocha Tukuyu
Na Mwandishi Wetu
HUENDA ule msemo wa maji hufuata mkondo ukawa na ukweli mkubwa. Mwimbaji na mmoja wa wamiliki na waasisi wa bendi ya Tukuyu Sound ama KP, Johnson Nguza ama maarufu kama Papii Kocha ameiacha bendi hiyo na kujiunga na Town Classic Band ya mjini Dar es Salaam.
Habari za uhakika ambazo Uelekeo inazo zinathibitisha kuwa Papii ambaye alikuwa na mshirika wake Kalala Hamza Kalala maarufu kama Kalala Junior, sasa hawataonekana katika jukwaa la Tukuyu pamoja na ni suala la muda kabla Town Classic kumtangaza yeye na wanamuziki wengine wawili kutoka katika bendi hiyo.
Inaelezwa Papii amesainishwa mkataba wa miaka miwili ambapo amepewa gari jipya aina ya Nissan Duals pamoja na pesa taslim sh milioni saba. Gari hiyo amekabidhiwa wiki sasa. Wakati Town Classic ikianza mwanamuzi Totoo Kalala alipewa sh milioni tano na gari IST ili kumng’oa Tukuyu.
Meneja wa Town, Andrew Sekidia amethibitisha kufanya mkutano wa utambulisho wa wanamuziki wapya bila kuwataja majina. Papii anaondoka Tukuyu akiambatana na mpiga bass Babaa na mpiga solo Ilombee Kichinja.
MAJI HUFUATA MKONDO:
Mwishoni mwa miaka ya themanini baba mzazi wa Papii, ‘Jenerali’ Nguza Vicking aliacha bendi yake aliyokuwa na hisa ya Marquiz Original na kwenda kuasisi Sambulumaa iliyokuwa ikimilikiwa na Emmanuel Mpangala ambaye wakati huo alikuwa mfanyakazi wa Shrika la Ugawaji ya Taifa (NMC).
Moja ya makubaliano ya kwenda Sambulumaa ilikuwa baada ya miaka miwili bendi hiyo ingekuwa mali ya Nguza jambo ambalo halikufanyika na mwanamuziki huyo kulazimika kujiondoa ambapo alikaa benchi kwa muda kabla ya kuajiriwa International Orchestra Safari Sound na kuibuka na mtindo wa Rashikanda Wasaa na kumfia mikononi.
Mwishoni mwa miaka ya 1990 Papii aliziingiza bendi tatu kwenye mgogoro. FM Muisica Internationale, Diamond Dound na Beta Musica.