WAPO wanaume wanaoona aibu kwamba akienda na mkewe kliniki watu watamuona ameshikwa masikio au ametawaliwa na mke.” Anasema Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Iyunga jijini Mbeya, Dk. Yusta Ndotela.
Dk.Yusta alikuwa anazungumzia ushiriki duni wa wanaume kwenye masuala ya afya ya uzazi ya wake zao jijini Mbeya.
Watalaamu wa tiba wanasema kwamba wanaume wengi wametawaliwa na dhana isiyo sahihi kwamba suala la ujauzito ni la mwanamke pekee, kwa vile ndiye anayeibeba lakini wanasema ushiriki wa baba wa muda wote katika afya ya ujauzito ni muhimu na kuna faida kubwa.
Kutokana na kutojua umuhimu wa ushiriki wao, wanaume wengi wamekuwa na visingizio lukuki alimradi wasiandamane na wake zao kliniki, lakini wataalamu hao wanasema visingizio vinavyotolewa si vya msingi ikilinganishwa na faida zinazopatikana kwa uwepo wao kwenye huduma za afya tangu mimba inatungwa hadi mtoto kukua.
Akitoa mfano kuhusu ushiriki duni wa wanaume, Dk. Yusta anasema takwimu za mwezi uliopita zinaonesha kwamba wanawake walioanza kliniki katika kituo hicho wakiwa na ujauzito wa umri wa chini ya wiki 12, walikuwa 12.Hata hivyo, waliokuja na wenzi wao walikuwa watatu tu.
“Kwa hiyo utaona mwamko bado ni mdogo. Mpaka sasa wajawazito wanaokuja na wenza wao kuanza kliniki ni chini ya wastani ya asilimia 25,” anasema.
Anasema wanaendelea kutoa elimu kwa wanaokuja kliniki wakishirikiana na watu wanaoitwa Mbata, ambao wanatoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa ushiriki wa wanaume kwenye huduma za afya za wenzi wao.
FAIDA ZA USHIRIKI WA WANAUME
Dk.Yusta anasema zipo faida nyingi za mwanaume kuongozana na mwenza wake kliniki wakati wa ujauzito.
“Kwanza ni muhimu kutambua mwanamke anapopata ujauzito jukumu la kutunza mtoto tangu akiwa tumboni, ni la mke na mume na siyo jukumu la mmoja pekee. Iwe kiafya, kisaikolojia mpaka atakapojifungua. Jukumu la kulea mtoto ni la wote,” anasema.
Anasema mwanaume unapofika hospitali ukiwa na mwenzi wako, faida ya kwanza ni kutunza afya.
“Faida ya pili mnapofika, wote mtapata ushauri nasaha, mtapimwa hali za afya na hii siyo tu maambukizi ya viusi vya ukimwi, bali yapo magonjwa mengine ambayo yanaweza kumpata mjamzito yakamdhuru mtoto au atakapojifungua akapata shida.
Magonjwa hayo ni pamoja na kaswende, ambayo baba anapaswa pia kujua na kushirikiana na mwenza wake kuyatibu.
Hivyo wakienda kliniki watapima wote wawili, kwa maana hiyo mkiwa katika hali salama mnajihakikishia kwamba mtoto atakuwa salama, kwa sababu hata mama anapokuwa mjamzito mtakuwa bado mnakutana katika tendo la ndoa,”.
Anataja faida nyingine ya baba kumsindikiza mkewe kliniki ni kujua kama ana matatizo yoyote yanayohitaji kula aina fulani ya vyakula au kuhitaji kutofanya kazi.
Anafafanua kwamba mara nyingi wanaume ndio watoaji wa mkate, anaposikia kutoka kwa daktari kwamba mwenza wake anatakiwa kula vyakula vya aina fulani, inakuwa vyema zaidi kuliko anapokuja kuambiwa baadae na mkewe.
“Tunapata kesi nyingi, mama amekuja kliniki anaambiwa anatakiwa kula aina fulani za vyakula. Anaporudi nyumbani na kumwambia mume wake, mume anamwambia unadeka na kumpa maneno yanayokatisha tamaa,” anasema.
Anataja jambo lingine muhimu kwa kina baba kujua, mjamzito anapoonekana anahitaji mapumziko ya muda mrefu (bed rest), kama kauli haitatolewa na daktari mumewe asiposikia mubashara, anawe¬za kudhani anataka kujidekeza.
“Kisaikolojia, mjamzito anaposindikizwa na mwenza anajisikia faraja kwamba waliutafuta ujauzito pamoja na wanapelekana hospitalini na kurudi nyumbani pamoja,” anasema.
Anasema mwanamke anapokuwa mjamzito anapata changamoto nyingi za kisaikolojia, hivyo ukaribu wa mwenza wake muda wote ni muhimu kwa faida ya mama na mtoto tumboni.
Faida nyingine kwa mujibu wa mtaalamu huyo, ni kusaidia kufanya maandalizi sahihi wakati wa kujifungua na baada, kwani takwimu zinaonesha kuwa wanawake wengi wanaohudhuria kliniki peke yao, maandalizi yao huwa duni ikilingan¬ishwa na wanaoongozana na wenza wao.
Anatoa wito kwa wanaume kubadilika na kuwa na mtazamo chanya juu ya kushiriki katika mfululizo wa ufikaji na wenza wao kliniki kutokana na faida lukuki zinazopatikana.
“Wanaume watambue kuwa kuitwa mzazi wa mtoto kunaanzia tangu maandalizi ya kutungwa kwa mimba mpaka malezi baada ya mtoto kuzaliwa,” anasema. Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Iyunga jijini Mbeya, Dk Yusta Ndotela
Ushiriki wa wanaume wakiwa na wenza wao wajawazito wanaohudhuria katika Kituo cha Afya Iyunga, hautofautiani na ule ulioanza kuon¬ekana katika kituo kipya cha afya cha Nzovwe kilichoanza kufanya kazi hivi karibuni jijini Mbeya.
Mganga Mfawidhi wa kituo hicho Dk. Leticia Mgeta anasema elimu inahitajika kwa wanaume kutambua umuhimu wa kushiriki kliniki na wenza wao.
Anasema akina baba wanaowasindikiza wenzi wao wajawazito kliniki ni wachache na anapotokea mmoja mmoja wanampongeza na kumtia moyo, ili awe chachu ya kuhamasisha wengine.
Akitoa taswira halisi ya Jiji la Mbeya juu ya ushiriki wa wanaume kwenye masuala ya uzazi, Mganga Mkuu Dk. Jonas Lulandala, anasema bado ushiriki uko chini na kwamba hilo ni tatizo linalohitaji nguvu ya pamoja ya wadau kulishughulikia.
“Tatizo lipo lakini tumejaribu namna ya kuanza kulipunguza ili wanaume waweze kushiriki kwenye masuala ya huduma za uzazi.
“Baba kama atashiriki kwenye suala zima la huduma ya uzazi akifika pale kliniki atapata elimu. Atajua ni lini wanaweza kuzaa yeye na mke wake, wazae watoto wangapi na wapange muda kati ya mtoto mmoja na mwingine,” anasema.
Mganga mkuu huyo anasema hali iliyopo ya umiliki wa uchumi kuwa chini ya wanaume katika familia nyingi, inaleta pia msukumo wa umuhimu wa mwanaume kuambatana na mkewe kwenda kliniki.
“Hii itawezesha wanaposimamia upangaji bajeti za familia wazingatie pia mahitaji ya msingi ya mama mjamzito” anasema.
Anaongeza “Kama tunavyofaharnu baba ndiye kiongozi wa familia akiwa wa kwanza kulifahamu hili, akashirikiana na mama itawezekana. Lakini kama mama peke yake ndiye atakuja kutoa elimu hii kwa baba, si akina baba wote watakubali kwa urahisi elimu anayoipata kwa mkewe.
“Lakini kitu kingine tunafahamu mama akishakuwa mjamzito, anahitaji mlo maalumu, ili uweze kumjenga kiafya yeye na mtoto aliyembeba tumboni. Suala hili litagusa uchumi.
Sasa tukiangalia uchumi katika familia mara nyingi anayeudhibiti ni baba hivyo kama baba atapata elimu pale pale kliniki, alikokwenda na mkewe ina maana hatohitaji nyumbani igeuke ajenda ijadiliwe tena,”.
Anasisitiza kuwa kitendo cha wanandoa kusindikizana kwenda kliniki kinaongeza upendo ndani ya nyumba.
Dk. Lulandala anasema wana¬chokifanya kwa sasa ni kuhamasisha kina baba kufika na akina mama hospitali ili wapate vipimo pamoja, kupata elimu na pia mama anayekwenda na mwenza anapewa kipaumbele kuhudumiwa kwanza, ili kuwapa morali zaidi wanaume waone hata wakienda hawakai muda mrefu.
Kusuasua huku kwa wanaume kwenye masuala ya afya ya uzazi kunaifanya Halmashauri ya Jiji la Mbeya kubuni mkakati madhubuti katika kuongeza ushiriki wa wanaume.
Mkakati huo ni kuwatumia madiwani na wenyeviti wa mitaa, kila mmoja kutoa elimu kwenye eneo analoliongoza.
Mohamed Issa Meya wa Jiji la Mbeya,a nasema haipendezi kuona wanaume wanaendelea kuwaachia wanawake jukumu la masuala ya afya ya uzazi. Anasisitiza kuwa ni wakati wa jinsi zote kushiriki ili kuwezesha kuwa na jamii yenye ustawi.
“Ni suala ambalo lipo na hata mimi linanisikitisha, kwa sababu mimi binafsi mke wangu amezaa watoto watano na siku zote nilikuwa ninakwenda naye hospitali, tangu mwezi wa kwanza tu anapopata ujauzito mimi na yeye mguu kwa mguu tunakwenda hospitali.
“Nitoe wito kwa kina baba wenzangu, kwamba mtoto wa kwetu wote. Ule mzigo tukimwachia mama peke yake si sahihi. Wakati wa ujauzito ni wakati wa kuwa naye karibu, umwonyeshe mapenzi.
Lakini katika hili kwakuwa ninao madiwani wenzangu, ambao wana wananchi kwenye kata zao nao naelekeza watoe elimu kwenye vikao vyao wazungumze hili,”anasema Issa.
“Wenyeviti wa mitaa wahamasishe kwa sababu siyo kwamba mama ukishampa ujamzito ndiyo basi umtelekeze hapana.Yule mtoto akizaliwa haitwi bin mama anaitwa bin baba,” anasema.
“Lakini pia ukiachana na nafasi yangu ya umeya kwa upande wa pili, nikiwa sehemu ya viongozi wa dini nawasihi pia viongozi wa dini zote kuhakikisha wanatumia nyumba zao za ibada kuielimisha jamii juu ya jambo hili.
Lisiishie kusisitizwa na wanasiasa pekee” anasistiza Meya huyo ambaye pia ni Shehe wa Msikiti mkubwa wa Isanga katika Jiji hilo la Mbeya.
Kwa upande wao wanaume wanasema kitendo cha wao kutokwenda kliniki kunasababishwa na majukumu mengi ya kifamilia waliyonayo, hivyo inakuwa vigumu wao kupata muda wa kuhudhuria kliniki wakiwa na wenzi wao.
Omary Abdu anasema yeye hajahawi kwenda hata siku moja, kutokana na kutingwa na makujumu ya kutafutia familia yake mkate wa kila siku, hivyo jukumu hilo kubaki kuwa kwa mke wake.
“Wengi wanatamani, lakini kutokana na baba kuwa ndiye mwenye jukumu la kutunza familia yake, inakuwa ni vigumu kuongozana na mke wake kwenda kliniki tukiamini kuwa kuongozana ni kama tunapoteza muda,”anasema Abdu.
Naye Hamis Tumbo amesema kitendo cha mke na mume kuongozana kwenda kliniki ni kizuri, lakini bado jamii hasusani upande wa wanaume hawana uelewa wa jambo hilo, hivyo ameomba serikali na wadau wengine kutoa elimu hiyo.
Na MWANDISHI WETU