NYOTA wa muziki wa dansi raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Fally Ipupa, leo anatarajia kutoa burudani ya aina yake kwa wakazi wa Mwanza na maeneo jirani.
Onyesho hilo litafanyika katika Hoteli ya Malaika, jijini Mwanza, ikiwa sehemu ya kumbukizi ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Akizungumza jijini humo, Fally Ipupa, ameahidi kutoa burudani ya aina yake na kukata kiu ya mashabiki wa muziki watakaohudhuria katika onyesho hilo.
Amesema anatambua mashabiki wa muziki wa Kanda ya Ziwa walikuwa wakisubiri burudani kwa muda mrefu, hivyo wajitokeze kwa wingi katika onyesho hilo.
“Nimejiandaa vizuri na kwamba ninatambua nina mashabiki wengi jijini Mwanza na maeneo ya karibu, hivyo nitatoa burudani ya aina yake,” amesema Fally Ipupa.
Meneja wa mwanamuziki huyo, Madina Djobongue, alisema amefurahishwa na mapokezi ya wadau na wapenzi wa muziki na kwamba watapata burudani ya nyimbo mbalimbali ambazo zipo katika albamu mpya ya ‘Tokos’.
“Show ya Mwanza itakuwa na mvuto zaidi ya ile ya awali ambayo tulifanya Dar es Salaam, hivyo tumejipanga vyema kutoa burudani safi,” alisema.
Alisema utamaduni wa wananchi wa Mwanza na ukarimu wao, umemvutia kiasi cha kufikiria kujenga makazi yake jijini hapa.
“Mwanza ni pazuri kwa mazingira ya kuishi, kuna watu wenye ukarimu kwa kiasi kikubwa, hivyo amepanga kujenga makazi yake katika eneo hili,” alisema.
Na BALTAZAR MASHAKA, Mwanza