BENKI ya Dunia (WB) mwishoni mwa mwaka huu imeidhinisha mkopo nafuu wa dola 500 milioni za Marekani (zaidi ya sh. trilioni 1.2 za Tanzania kwa ajili ya kuboresha barabara na viwanja vya ndege nchini.
Mkopo huo utasaidia kujenga na kukarabati barabara zenye urefu wa jumla ya kilomita 500 ikiwamo ya kutoka Mtwara mpaka Masasi kupitia Mingoyo yenye urefu wa kilomita 201.
Hizi ni habari njema kwa wakazi wa mikoa miwili inayopakana ya Mtwara na Lindi.Ni habari njema kwa sababu uimara wa barabara unakuza uchumi na hivyo kuwezesha wananchi kusonga mbele kwa maendeleo.
VIJIJI HUSIKA
Ukarabati wa barabara hii ya Mtwara hadi Masasi ambayo inapitia katika vijiji vya Mkoa wa Mtwara ukiwemo mji mdogo wa kale na wa kitalii wa Mikindani na kufuatiwa na vijiji vya Mbuo, Ndumbwe, Mpapura na Namnamba kilichopo kwenye mpaka wa mkoa wa Mtwara na Lindi.
Kuanzia hapo katika mkoa wa Lindi unapita katika vijiji vya Madangwa, Mnolela , Namunda, Likokwe, Mkwaya, mji mdogo wa Mnazi Mmoja(Mingoyo) Mahumbika, Kiwalala, Mtua, Nyengedi, Mtama (wilaya ndogo), Nyangao hadi kijiji cha Nkungumahiwa kwenye mpaka mwingine wa mikoa ya Mtwara na Lindi.
Kijiografia mikoa ya Lindi na Mtwara ina mipaka maeneo mawili mpaka wa kwanza upo katika barabara ya kutoka Mtwara mjini kwenda Mnazi Mmoja(Mingoyo) katika kijijicha Namnamba.
Mpaka wa pili wa mikoa hiyo upo katika kijiji cha Nkungumahiwa katika barabara kutoka Mnazi Mmoja kwenda Masasi, wilaya iliyopo katika mkoa wa Mtwara. Wilayani Masasi katika barabara hiyo kuna vijiji vya Nangoo,Nanganga, Chipite, Ndanda,Chikundi,Chigugu, Chikukwe,Namakongwa,Maili Sita,Mtandi hadi Masasi mjini.
VIKUNDI VYA UZALISHAJI
Hii ni fursa kwa wananchi katika vijiji kando ya barabara hii ambayo serikali imesema itaikarabati. Ni fursa kwao kubuni miradi midogo midogo wakiwa katika vikundi ama mmoja mmoja ili barabara iweze kuwaletea maendeleo. Barabara ya Mtwara hadi Masasi inapitia katika vijiji ambavyo vina rutuba na bonde la mto Lukuledi.
Baadhi ya vijiji vina mashamba ya minazi,korosho, mihogo, na katika bonde la mto Lukuledi kuanzia Mahiwa hadi Mkwaya mkoani Lindi linafaa sana kwa kilimo cha aina mbali mbali za mboga zikiwemo nyanya.
Aidha, katika wilaya ya Masasi inamopita barabara hii kuna bonde la Chigugu ambapo wananchi wanajishughulisha kwa kilimo cha mboga tofauti, nyanya, mchicha na nyinginezo.
Kinachotakiwa sasa wananchi pembezoni mwa barabara hii ya urefu wa kilomita 201 watumie fursa kupanua shughuli zao za kiuchumi.
Wanaohusika na kilimo cha korosho,nazi,miwa katika eneo la Kiwalala na mboga katika mabonde wajitahidi kuongeza uzalishaji maradufu kwa kuwa njia ya uhakika ya kusafirisha mazao kwenda masoko mbali mbali nchini na nje ya nchi imepatikana kwa ukarabati wa barabara.
Kwa kuwa vijiji vingi kwenye barabara ya Mtwara hadi Masasi kupitia Mnazi Mmoja(Mingoyo) tayari vina umeme,ni jambo jema kwa wananchi kuungana katika vikundi na kuanzisha viwanda vidogo vya kuchakata mazao yao na kuyasafirisha kuyapeleka kwenye masoko katika miji ya mikoa yao ya Lindi na Mtwara.
MASOKO YA UHAKIKA
Masoko mengine ya uhakika ni jiji la Dar es Salaam ambalo idadi ya wakazi inaongezeka karibu kila siku na huenda sensa itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu itaonyesha dhahiri ongezeko la idadi ya watu hadi milioni sita kutoka milioni 4.365 ya sensa ya miaka 10 iliyopita mwaka 2012.
Soko lingine la uhakika kwa bidhaa na mazao ya wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara lipo nchi jirani ya kisiwa cha Comoro ambacho kinategemea sana mazao ya chakula ikiwemo mihogo ambayo inalimwa sana Masasi,nazi, vitunguu na nyama kutoka Tanzania.
Viongozi wa mikoa ya Mtwara na Lindi waendelee kuwahamasisha wananchi katika uzalishaji hasa wakiwa katika vikundi ili barabara inayokarabatiwa kutoka Mtwara kupitia Mnazi Mmoja (Mingoyo) hadi Masasi iwe ya manufaa kiuchumi kwa wananchi na mikoa hii miwili.
Mwandishi wa makala ni mwanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) anapatikana email nakajumoj@ gmail.com na Whatsapp 0784291434.