BODI ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, imeingia makubaliano na Kampuni ya Twiga Foods Limited ya Kenya ili kufanya biashara ya pamoja kwa mazao ya nafaka.
Makubaliano hayo yanafungua ukurasa mpya katika soko la nafaka kati ya Kenya na Tanzania ili kuleta tija kwa wakulima na wazalishaji wa nafaka nchini, ambao wanazalisha kwa wingi ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Twiga Foods Limited ya Kenya, Yabeltal Getachew, Mkurugenzi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Dk. Anselm Moshi, alisema bodi hiyo, imeendelea kupanua wigo wa masoko kwa kufanya kazi na wafanyabiashara mbalimbali Afrika Mashariki ili kujenga soko imara.
“Nimefanya ziara hii ya kikazi jijini Nairobi katika jitihada za kupanua masoko ya mazao ya wakulima wetu, lengo la kutembelea kampuni ya Twiga Foods Limited ni kufanya mazungumzo nao na kujenga msingi wa kibiashara kati ya nchi zetu mbili ili wakulima wetu, wasihangaike kutafuta masoko ya kuuza mazao yao,” alisema.
Aliongeza kuwa, walikwenda Kenya kwa mwaliko wa Kampuni ya Twiga Foods Limited ili kuangalia miundombinu yao kwa ajili ya kupokea, kuhifadhi na kusambaza nafaka ambazo zinazalishwa na Bodi ya Mazao Mchanganyiko.
Aidha, Dk. Moshi alifafanua kuwa, kampuni hiyo ina miundombinu ya kisasa ya kupokea, kuhifadhi na kusambaza nafaka zikiwemo roboti mbalimbali jambo ambalo limeivutia bodi hiyo kufanya nayo kazi ikiamini kutakuwa na ufanisi mkubwa.
Alisema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuzalisha nafaka na mazao mengine kama kunde, mtama, mboga, mazao ya matunda na maua, hivyo aliahidi kufanya nayo kazi kwa manufaa ya nchi hizo mbili.
“Jambo kubwa ambalo wao wamelieleza ni kumfikishia mlaji chakula kwa bei nafuu zaidi, kwa mtazamo wetu, hili ni jambo muhimu kwamba, mlaji apate chakula kwa bei nafuu na kiasi kingine cha fedha zake, akitumie katika shughuli za maendeleo,” alisema Dk. Moshi.
Alisema makubaliano hayo ni matunda ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini humo Mei 6, mwaka huu ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kufungua milango na kuimarisha uhusiano.
Katika ziara hiyo, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa Kenya na Tanzania kushirikiana bila kuwepo ushindani, kauli au vitendo vya kukwazana.
Kwa upande wake, Getachew alisema amefurahishwa na ujio wa mkurugenzi huyo na kwamba, wako tayari kufanya na biashara kwa kuwa wana uhakika wa kupata bidhaa kwa wakati na ubora unaohitajika.
Na MWANDISHI WETU



























