Na MWANDISHI WETU
SIKU moja baada ya kuanza shindano la kutafuta staa mwenye vioja na mvuto Afrika Mashariki, msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Gift Stanford ‘Gigy Money’ amesema anaishi maisha huru ya kutoogopa kusema ukweli.
Gigy alitoa kauli hiyo juzi jijini Nairobi ambapo kunafanyika shindano hilo baada ya kugombana na mshiriki kutoka Uganda.
Msanii huyo anayetajwa kuwa na vituko na maneno mengi alisema maisha anayoishi ni halisi na hapendi kufanya maigizo na ndio maana anapokwazwa huamua kutoa ya moyoni.
Gigy, mama wa mtoto mmoja alisema huenda akachukiwa na kutengwa katika shindano kwani atalazimika kugombana na kusema ukweli pindi atakapokosewa.
“Maisha ninayoishi humu ndiyo maisha yangu halisi ninayoishi siku zote, sipendi mtu anikwaze, nitasema ukweli pindi nitakapokosewa na sipo tayari kunyamaza kwa ajili ya kutafuta amani ya moyo wangu,” alisema Gigy.
Shindano hilo lililoanza juzi, linashirikisha wasanii na watu wengine maarufu kutoka nchi za Kenya, Tanzania na Uganda.
Kila nchi inawakilishwa na wasanii wanne na mshindi kwenye shindano hilo atajishindia mamilioni ya fedha.
Staa huyo amekwenda kushiriki shindano hilo ikiwa ni miezi miwili baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), kumfungia kufanya kazi za muziki ndani na nje ya nchi.
BASATA ilimfungia Gigy baada ya kufanya onyesho la moja kwa moja lililoacha maungo yake wazi ambalo ni kinyume na maadili ya Kitanzania.