WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima, amesema mapambano endelevu wa kijinsia, ni moja kati ya maeneo matatu yatakayowekewa mkazo na wizara yake.
Amesema lengo ni kuhakikisha serikali inatoa nafasi kwa wanawake kuwa na mazingira mazuri ya kustawi kijamii na kiuchumi. Dk. Dorothy alisema maeneo mengine ni usawa katika upatikanaji wa fursa za kiuchumi serikalini na elimu ya maelewano baina ya wanawake na wanaume nchini kupitia mpango kabambe alioutambulisha kwa jina la ‘He4She’.
Waziri Dk. Gwajima ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam, katika hafla ya Jukwaa la Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC), iliyoambatana na uzinduzi wa Ripoti ya Utafiti wa Ushiriki wa Wanawake na Makundi Maalumu katika Manunuzi ya Umma.
Mosi alisema serikali ya Rais Samia, imekuwa mstari wa mbele kuandaa mazingira wezeshi ya kumkomboa mwanamke, lakini fursa nyingi zimekuwa zikibaki kwa wachache waliopo mijini, huku kundi kubwa ambalo linabeba asilimia kubwa ya uzalishaji mali katika shughuli za kilimo, likibaki bila taarifa sahihi vijijini.
Waziri Dk. Gwajima alisema mwaka 2016 serikali ilifanya mabadiliko ya Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka ya 2011, katika Kifungu cha 64 (a) kipengele cha 2, kwa kutoa nafasi kwa makundi maalumu.
Alisema lengo la mpango huo, ilikuwa ni kuwawezesha kushiriki katika fursa za manunuzi ya umma iliyotaka kutengwa kwa asilimia thelathini ya bajeti yake ya manunuzi kwa ajili ya makundi maalumu wakiwepo wanawake.
Pia alisema kila mwanamke aliyepata nafasi ya kufahamu kuhusu fursa za kiuchumi zilizopo kwa ajili ya wanawake, ahakikishe anakuwa mstari wa mbele katika kuwafikia wanawake wengine walioko vijijini, ambao wamekuwa wakipitwa na fursa mbalimbali kutokana na mazingira yao hali inayodumaza jitihada za kumkomboa mwanamke.
Alitumia fursa hiyo kutangaza kuunda Kamati maalumu ya kuwafikia wanawake kote nchini, yeye akiwa Mjumbe wa kamati hiyo, itakayoongozwa na TWCC na wadau wengine binafsi na kiserikali, ambao majukumu yao makubwa ni kuwawezesha wanawake katika jamii.
Pia alisema katika eneo la utoaji wa mikopo ya asilimia 30 kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu katika kila halmashauri utekelezaji umekuwa mdogo, kiasi cha kuyakwamisha makundi hayo kwa makusudi.
Aliagiza kila halmashauri kuwajibika katika utekelezaji wa sheria hiyo ili malengo ya serikali kwa makundi hayo yafikiwe kikamilifu, kwa maslahi ya taifa na watu wake.
Pili, alisema suala la unyanyasaji wa kijinsia limekuwa tatizo sugu, ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya wanawake katika jamii, hivyo kuagiza kila mwananchi kutofumbia macho vitendo vya aina hiyo ambavyo matokeo yake ni mabaya.
Waziri huyo alitolea mfano wa mauaji ya mke na baadaye mume kujiua mkoani Mwanza, wiki kadhaa zilizopita, kwa kusema uchunguzi ulibaini kabla ya vifo vya wanandoa hao, kulikuwa na viashiria vyote vya unyanyasaji wa kijinsia.
Alisema inawezekana jamii haikutoa taarifa hizo katika mamlaka zinazotakiwa, jambo ambalo limesababisha vifo kwa wanandoa, hivyo kutoa wito kwa jamii kutoficha taarifa muhimu ili kuokoa maisha ya watu miongoni mwa jamii.
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti iliyowasilishwa na Dk. Donath Olomi, asilimia kubwa ya taasisi za serikali hazitengi bajeti ya kuwawezesha wanawake na makundi maalumu katika manunuzi ya umma, wakati serikali imeweka bayana kuhusu umuhimu huo kwa kuagiza kutengwa kwa asilimia 30 ya bajeti katika kila mwaka wa fedha.
Na WILLIAM SHECHAMBO