Aanza na watumishi waliokubali kurudisha sehemu ya mamilioni yaliyotafunwa kutokana na wizi huo
Na ANITA BOMA, SONGWE
WAZIRI wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima, amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, kuwachukulia hatua watumishi wote wa afya mkoani humo, waliohusika na wizi wa dawa zenye thamani ya sh. milioni 13.5 na kurudisha milioni 10.6.
Ameagiza watumishi hao kufikishwa kwenye vyombo vya uchunguzi, ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na polisi ili uchunguzi ufanyike kabla hatua zaidi za kisheria hazijafuata.
Dk. Gwajima, alitoa agizo hilo juzi, baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo, kuhusu huduma za afya, iliyowasilishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Hamadi Nyembea, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kikazi ya siku moja ya waziri huyo kukagua mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na kuangalia hali ya utoaji wa huduma za afya.
Alisema haiwezekani watumishi wa afya waibe dawa halafu warudishe fedha bila ya kuchukuliwa hatua yoyote, kwa kuwa kwa kufanya hivyo, wameonyesha kuwa siyo waadilifu, wameshindwa kuheshimu mali ya umma na kusababisha hasara kubwa ya bidhaa muhimu za dawa.
“Haiwezekani warudishe tu fedha halafu iishie hapo, warudishe halafu wakueleze namna wanavyoiba na kisha uwapeleke kwenye vyombo vya sheria kama PCCB (TAKUKURU) na Polisi, halafu nao wawaeleze hizo mbinu wanazotumia, baada ya hapo mahakamani. Baada ya hatua hizo, bado tutarudi utumishi kuwauliza je, hawa watu wanafaa kuendelea kuhudumu katika wizara hii?” Alisema.
Aliongeza kuwa watumishi hao kulipa au kurudisha baadhi ya fedha hizo ni kuonyesha kuwa, tabia hiyo ya wizi wa dawa imekomaa miongoni mwao, hivyo mkoa wa Songwe, hauna budi kuendelea na ukaguzi zaidi kwani kwa anaamini ukaguzi wa dawa uliofanywa katika ngazi ya mkoa, kama ungefanyika na nje ya halmashauri, kuna uwezekano ingepatikana hesabu kubwa zaidi ya upotevu wa dawa.
“Sasa natangaza vita ya wadokozi wa bidhaa za afya, vyombo vyote vya kisheria vitahusika na vita dhidi ya wabadhirifu wa bidhaa za dawa, maana wapo watumishi wachache wanarudisha nyuma ugavi wa bidhaa za dawa na kushindwa kusimamia vyema mali ya serikali,” alisisitiza.
Waziri huyo, aliwataka watumishi wa afya mkoani humo, kuwa wasimamizi katika kuhakikisha huduma ya dawa inapatikana sawasawa na hakuna wizi unaofanyika, huku akitaka kila mmoja kuwa mlinzi kwa mwenzake katika kuwabaini wenye tabia za udokozi wa dawa, bila kujali muhusika ni nani kwake.
“Lengo la serikali ni kuona watumishi wote wanaofanya mchezo huo mchafu, wanachukuliwa hatua za kisheria ili wafikishwe kwenye bodi na mabaraza ya kitaaluma, kwa ajili ya kuchukuliwa hatua kulingana na mabaraza hayo,” alisema.
Dk. Doroth, alisema haiwezekani Rais Dk. John Magufuli, anajitahidi kuhakikisha upatikanaji wa dawa unaboreka, halafu wanatokea watu wachache wanarudisha nyuma jitihada hizo.
TAARIFA YA MKOA
Awali, akisoma taarifa ya mkoa kuhusu utoaji huduma za afya, Mganga Mkuu wa mkoa, Hamadi Nyembea, alisema Songwe imeongeza jitihada kudhibiti upotevu wa dawa kwa kuimarisha ukaguzi wa mara kwa mara katika vituo vya kutolea huduma.
Alisema ukaguzi umekuwa ukifanyika kwa kuwahusisha wakaguzi wa ndani kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri, ambapo katika mwaka wa fedha 2020/21, jumla ya vituo 103, sawa na asilimia 53.4, vilifanyiwa ukaguzi wa dawa kubaini upotevu wa dawa zenye thamani ya sh. milioni 13.5, ambapo watumishi waliohusika walitakiwa kurejesha fedha hizo, wakafanikiwa kurudisha sh. milioni 10.6.
Dk. Nyembea, aliongeza kuwa kutokana na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, mkoa umebaini kuwa mnyororo wa bidhaa hiyo umeanza kuimarika na upotevu wa dawa katika vituo vilivyofanyiwa ukaguzi umepungua kwa kiwango kikubwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela, alimuahidi waziri huyo kuwa, maagizo ya kuhakikisha watumishi waliohusika na wizi wa dawa na kuiingizia hasara serikali wanafikishwa kwenye vyombo vya kisheria, yatatekelezwa haraka iwezekanavyo.