WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, amewaonya wanaopotosha hotuba za viongozi kuhusu kampeni ya hiyari ya chanjo ya kupambana na mlipuko wa homa ya kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona (Uviko 19).
Aidha, amesema wizara yake itakuwa mstari wa mbele kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kutekeleza kampeni iliyotangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kuchanja kwa hiyari, ili kuwanusuru Watanzania na mlipuko wa ugonjwa huo.
Dk. Gwajima ametoa kauli hiyo, wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa mashirika yasiyo ya kiserikali, siku moja kabla ya uzinduzi wa mkutano huo, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais, Samia Suluhu Hassan. Mkutano huo umeandaliwa na Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO).
Amesema ni vizuri kujiridhisha kama umeelewa vizuri kilichosemwa katika hotuba ya kiongozi, kabla ya kuandika au kuamua kuzungumza au kuandika chochote kuhusiana na umuhimu wa suala hilo.
“Bahati nzuri wale waliopotosha wameshaomba msamaha, hivyo tujitahidi kuwa makini, kampeni kubwa ya kuwaelemisha watu ikifanyika itasaidia watu kukata shauri kwa imani yao na kwa hiyari,” alisema.
Alisisitiza kuwa, katika kampeni hiyo ambayo Rais Samia aliagiza ifanyike kwa kutoa elimu, wizara itashirikiana na wadau wote, yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali katika kuitekeleza wakitumia mwongozo maalumu ambao utawezesha mashirika kutoa elimu katika maeneo yaliyopo katika halmashauri, ikiwemo mikoa, wilaya, kata na vijiji.
Akizungumzia mashirika yasiyo ya kiserikali, Dk. Gwajima alisema wizara hiyo itaendelea kuyawekea mazingira wezeshi ili yatekeleze majukumu ya kusaidia jamii ya Watanzania kwa kuzingatia sera ya taifa ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya mwaka 2001.
Nyingine ni Sheria namba 24 ya mwaka 2002 na marekebisho yake pamoja na kanuni, miongozo ya sheria nyingine za nchi bila kusahau misingi ya uzingatiaji wa misingi ya uwazi na uwajibikaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NACONGO, Dk. Lilian Badi, alisema baraza hilo limekusudia kuelimisha NGO ziiletee nchi maendeleo, hususan katika sekta ya afya.
Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii), Dk. John Jingu aliyataka mashirika hayo kutumia mkutano huo kujadili na kubaini mafanikio na upungufu ulioyojitokeza kipindi kilichopita, ili kuyatafutia ufumbuzi.
Katika hatua nyingine, Dk. Gwajima alizindua mwongozo wa sera ya nyongeza ya ushirikiano wa majukumu baina ya kada za afya kuhusu ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na ujazaji wa fomu namba tatu ya polisi (PF3), huku akiwataka watoa huduma kutumia maelekezo yaliyomo kutokomeza suala hilo.
Mwongozo huo unatoa mfumo wa huduma bora na toshelezi zinazojumuisha matibabu, rufaa, huduma za msaada wa kisaikolojia na kijamii zinazohusiana na ulinzi wa kisheria kwa watu wanaopatwa na ukatili wa kijinsia.
Na HAPPINESS MTWEVE, Dodoma



























