LIGI Kuu Tanzania Bara msimu huu imefikia ukingoni, bado mchezo mmoja kwa kila Klabu kabla ya ligi hiyo kumalizika.
Michuano hiyo ambayo tayari Yanga imetwaa ubingwa ilikuwa na ushindani mkubwa, kila timu ilihitaji kufanya vyema.
Licha ya washambuliaji wengi kuonyesha ubora wa kufumania nyavu, lakini makipa nao walionyesha uwezo mkubwa wa kulinda nyavu zao zisitikiswe.
Katika michuano hiyo, makipa mbalimbali wameonyesha ubora wa kuzuia mashambulizi na kufanikiwa kuwa kikwazo cha washambuliaji.
Makala hii inataja makipa kadhaa walioonyesha ubora msimu huu na kufanikiwa kutoruhusu bao katika michezo mbalimbali.
DJIGUI DIARRA (YANGA)
Moja kati ya usajili bora walioufanya Yanga kabla ya kuanza kwa msimu, basi ni kumpata kipa Djigui Diarra kutoka Mali.
Kipa huyo wa timu ya taifa ya Mali amekuwa na kiwango bora msimu huu na kuwa moja kati ya mchezaji aliyeongeza uimara ili kuhakikisha Yanga inajilinda vyema.
Diarra ndiye kipa aliyefanikiwa kutoruhusu bao katika michezo mingi kuliko kipa yoyote wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu hadi sasa.
Wakati ukibaki mchezo mmoja, Diarra amefanikiwa kutoruhusu bao katika michezo 15 ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kufanikiwa kushika nafasi ya kwanza.
ABUTWALIB MSHERY (YANGA)
Abutwalib Mshery ni mmoja kati ya makipa wazawa waliofanya vyema katika Ligi Kuu Bara msimu huu. Hadi sasa katika michuano hiyo amefanikiwa kutoruhusu bao katika michezo 11.
Kipa huyo alisajiliwa na Yanga katika usajili wa dirisha dogo msimu huu akitokea katika kikosi cha Mtibwa Sugar kutoka mkoani Morogoro.
Ingawa alianza kuonyesha ubora katika kikosi cha Mtibwa Sugar katika mzunguko wa kwanza, lakini bado kipa huyo ameendelea kuonyesha ubora mkubwa pale anapopata nafasi ya kucheza katika kikosi cha Yanga.
Kipa huyo ni chaguo la pili katika kikosi hicho, baada ya kipa chaguo la kwanza ambaye ni Diarra.
AISHI MANULA (SIMBA)
Kipa bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, Aishi Manula ni mmoja kati ya wachezaji muhimu zaidi katika kikosi hicho.
Ingawa hakuwa na msimu mzuri kama aliokuwa nao msimu uliopita, lakini anabaki kuwa ni mmoja kati ya makipa bora katika Ligi Kuu Bara msimu huu.
Kipa huyo namba moja wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, amefanikiwa kutoruhusu kufungwa bao katika michezo 11 ya Ligi Kuu Bara.
Kabla ya mchezo wa jana, Manula amekosekana katika michezo kadhaa iliyopita, akimpisha kipa mwenzake Beno Kakolanya ambaye naye amekuwa katika kiwango kizuri.
SAID KIPAO (KAGERA SUGAR)
Ushindi wa bao 1-0 iliyopata Kagera Sugar dhidi ya Coastal Union juzi, umemfanya kipa huyo kuwa mmoja kati ya makipa wasioruhusu kufungwa katika michezo mingi.
Mlinda lango huyo wa zamani wa JKT Ruvu, msimu huu amekuwa chaguo la kwanza katika kikosi cha Kagera Sugar chenye maskani yake jijini Bukoba.
Kipao amekuwa bora msimu huu akifanikiwa kutoruhusu bao katika michezo minane katika kikosi hicho kinachonolewa na kocha Francis Baraza.
Kagera Sugar inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi 38 katika michezo 29, imeshinda mechi tisa, sare 11 na imefungwa michezo tisa.
Miamba hiyo imefanikiwa kufunga mabao 20 na kuruhusu mabao 25 katika Ligi Kuu Bara hadi sasa.
WENGINE WALIOTISHA
Kipa wa Biashara United, Cleo Settuba na Metacha Mnata aliyekuwa akikipa Polisi Tanzania wameonyesha ubora mkubwa msimu huu.
Mnata ambaye hajaitumikia Polisi katika michezo kadhaa iliyopita na Settuba wamefanikiwa kutoruhusu bao katika michezo minane ya Ligi Kuu Bara hadi sasa.
Makipa wengine waliofanya vyema katika ligi kuu ni Mussa Mbisa wa Coastal Union ambaye hajaruhusu bao katika michezo saba na Hamadi Kadedi (7).
Na ABDUL DUNIA