TANZANIA imeendelea kuandika historia nyingine katika maendeleo ya sekta ya utalii, ambapo watalii 115,198 wametembelea maeneo ya vivutio vya utalii kwa kipindi cha miezi miwili kuanzia Aprili hadi Mei mwaka huu na kuingiza mapato ya sh. bilioni 15.5.
Aidha, mashirika makubwa ya kimataifa ya ndege yakiwemo EUROWING, ambalo ni mwanachama wa Lufthansa Group limeanza safari za moja kwa moja kutoka Frankfurt, Ujerumani hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), huku kampuni ya ndege ya Edelweiss ya Uswisi nayo imerejesha safari zake za moja kwa moja kutoka Zurich hadi KIA.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alibainisha hayo jijini Dodoma, alipokuwa akitoa taarifa yake kwa waandishi wa habari, kuhusu masuala mbalimbali ambapo amesema mafanikio hayo ni baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kurekodi filamu ya The Royal Tour.
Kwa mujibu wa Msigwa matokeo ya kazi hiyo iliyofanywa na Rais Samia, yameanza kuonekana kwani idadi ya watalii imeongezeka kwa kasi katika maeneo ya vivutio vya utalii na hoteli.
“Takwimu kutoka Hifadhi za Taifa (TANAPA) zinaonyesha Aprili na Mei mwaka huu,, idadi ya watalii waliotembelea maeneo yetu ya hifadhi 22 yanayojumuisha Serengeti, Manyara, Mikumi, Nyerere, Udzungwa na Ruaha, imeongezeka kufikia watalii 115,198, ambapo kati yao watalii wa ndani 71, 593 na watalii wa nje 43,605, ikilinganishwa na watalii 59,664 waliofika katika kipindi kama hicho mwaka jana ambapo watalii wa ndani walikuwa 46,624 na watalii wa nje 13,040.
Msigwa alisema: “Ongezeko hili pia limeongeza mapato kutoka sh. bilioni 5.7 hadi kufikia sh. bilioni 15.559. Hifadhi ya Eneo Maalumu la Ngorongoro takwimu zinaonyesha katika kipindi cha Aprili na Mei mwaka huu, idadi ya watalii imeongeza kufikia 51,044, ambapo wa ndani walikuwa 25,150 na watalii wa nje walikuwa 25,894, ikilinganishwa na watalii 22,954 katika kipindi cha Aprili na Mei mwaka jana.”
Amesema mapato kutoka Ngorongoro kwa kipindi hicho yameongezeka kutoka sh. bilioni 2.585 hadi kufikia sh. bilioni 10 sawa na ongezeko la asilimia 289.
SAFARI ZA NDEGE
“Tumeanza kupokea ndege za moja kwa moja kutoka nchi mbalimbali na juzi mmeona kampuni ya EUROWING, ambayo ni mwanachama wa Lufthansa Group, imeanza safari za moja kwa moja kutoka Frankfurt Ujerumani hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
“Ndege hii itakayokuwa inakuja moja kwa moja ina uwezo wa kubeba abiria 302 na itakuwa ikifanya safari mbili kwa wiki.
Kampuni ya ndege ya Edelweiss ya Uswisi, nayo imerejesha safari zake za moja kwa moja kutoka Zurich hadi Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) na inafanya safari mbili kwa wiki,” alifafanua.
Msingwa amesema kampuni hiyo kubwa yenye ndege 14 na ni mwanachama wa Lufthansa, imeanza kuleta ndege aina ya Airbus A 343 yenye uwezo wa kubeba abiria 314.
“Habari njema ni kwamba baada ya kusitisha safari zake za moja kwa moja kutoka Instabul hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), tangu Julai mwaka jana, kampuni ya Turkish Airline itarejesha safari zake kuanzia tarehe 21 Juni, 2022.
Aliongeza kuwa: “Hizi ni safari mahususi kabisa kwa ajili ya kuleta watalii, bila shaka nyote mnafahamu kuwa Turkish Airline, inafanya safari zake za moja kwa moja hapa nchini ikitua katika viwanja vya ndege vya kimataifa vya Dar es Salaam na Zanzibar.”
Msigwa alisema miruko ya ndege KIA imeongezeka kwa kasi kwani hadi kufikia Juni mosi mwaka huu, kulikuwa miruko 134, lakini kwa siku hizi chache za mwezi huu miruko ya ndege imeongezeka hadi kufikia 178.
“Baada ya filamu ya Royal Tour, matarajio yetu kwamba tunakwenda kuandika rekodi, ambayo haijawahi kufikiwa na nchi hii ya kupokea idadi kubwa ya watalii,” alisisitiza.
AONYA WAZUSHI LOLIONDO
Msemaji huyo Mkuu wa serikali, amesema serikali imeanza kufuatilia watu waliohusika kutoa taarifa za upotoshaji katika uwekaji alama za mipaka ya kutenganisha eneo la makazi na hifadhi la Loliondo na kuzua vurugu zilizosababisha kifo cha askari polisi.
Amesema askari huyo alipoteza maisha kwa kuchomwa mshale wa kichwa baada ya kuzuka vurugu baina ya wataalamu wa serikali waliokuwa wakiweka alama za mipaka katika eneo la Loliondo na wakazi wa eneo hilo.
Kulingana na Msigwa vyombo vya dola vipo katika uchunguzi kubaini wahusika waliotoa taarifa za upotoshaji, ambazo zilisababisha wananchi kuwavamia wataalamu wa serikali ambao walikuwa wakiweka mipaka katika eneo hilo.
“Vyombo vya dola hivi sasa vinafanya uchunguzi kubaini watu ambao wamehusika katika kutoa taarifa za upotoshaji zilizosababisha vurugu na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Hatua kali zitachukuliwa bila kujali cheo cha mtu kwa sababu nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa sheria na hatukatazi mtu kutoa taarifa, lakini kuposha au kufanya uchochezi ni kosa hatuwezi kumvumilia mtu wa aina hiyo,” alisisitiza
Alisema kitu ambacho Watanzania wanapaswa kufahamu ni kwamba hakuna askari ambaye serikali imemtuma kwenye eneo hilo, kuwatoa wananchi bali kilichokuwa kinafanyika ni kuweka mipaka kati ya eneo la makazi na hifadhi.
Msigwa alisema jambo la kuweka mipaka siyo geni na wala siyo mara ya kwanza kwa serikali kufanya hivyo na tayari imefanya katika maeneo mengine kwa nia njema.
“Nashukuru waandishi wa habari hamjatumika katika hili la kuichafua serikali yetu kuonekana kuwa juhudi alizofanya Rais ni bure za kutangaza na kuvutia watalii ili watu washindwe kuja kwa kuhofia usalama wa eneo husika, lengo letu ni kulinda ikolojia ya Serengeti ili kuendelea kupata fedha kutoka kwa watalii lakini pia kulinda wananchi wetu.
“Picha zenyewe ambazo zimesambazwa kwenye mitandao ni za siku nyingi, lakini pia kuna taarifa ni za eneo lingine kabisa, hivyo uchunguzi utakapokamilika na watakaobainika hatua kali zitachukuliwa kukomesha suala hili.”
MIRADI YA KIMKAKATI
Akizungumzia miradi ya kimkakati, Msigwa alisema serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara, madaraja na vivuko kwa ajili ya kuwawezesha Watanzania kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kukuza uchumi. Alisema miradi yote ya ujenzi inaendelea vizuri, kwani wakandarasi wanalipwa fedha zao kadiri wanavyokamilisha kazi husika.
“Serikali inaendelea kujenga mradi mkubwa wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (SGR) Dar es Salaam – Morogoro, tumefikia asilimia 95, Morogoro – Makutupora tumefikia asilimia 90, Makutupora – Tabora, ndio kwanza tumeanza na sasa tumekamilisha maandalizi ya ujenzi wa kipande cha Tabora – Isaka, wakati wowote tutatiliana saini mkataba wa ujenzi na mkandarasi atakayejenga kipande hiki,” alisema.
Kuhusu ujenzi wa mradi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere, Msigwa amesema, mradi unaendelea vizuri, mpaka sasa ujenzi kwa ujumla umefikia asilimia 62.95 na mpango uliopo ni kukamilisha mradi huo ifikapo Juni 2024 .
Amebainisha kuwa, ujenzi wa bwawa hilo, unakwenda sambamba na ujenzi wa njia za kusafirishia umeme kutoka ulipo mradi kwenda Chalinze utakapoungana na Gridi ya Taifa na pia kujenga vituo vya kupoozea umeme.
Msigwa ameeleza kwamba pamoja na mradi huo, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), inaendelea kutekeleza miradi mingine ya kuwahakikishia Watanzania umeme wa uhakika wakati wote, ikiwemo wakati wa ukame ambapo vyanzo vya kuzalisha umeme kwa kutumia maji hupunguza uzalishaji.
“Natambua kuwa wiki hii kuna uzushi ulitengenezwa kwamba serikali imepandisha bei ya umeme kinyemela nawaomba Watanzania tupuuze uzushi huo, hakuna bei ya umeme iliyopandishwa viwango vipo vilevile ambavyo vilipangwa tangu miaka mingi.” Alieleza
“Viwango vinavyotozwa ni sh. 356.24 kwa uniti moja kwa kundi la matumizi ya jumla na linajumuisha wateja wa majumbani, biashara za kati, taa za barabarani, mashine pia kuna kundi la wateja wenye matumizi madogo ambapo bei yao ni sh. 122 kwa uniti moja.”
Aidha, Msigwa alisema serikali inatekeleza awamu ya pili ya ujenzi wa majengo ya Mji wa serikali, ambapo itatumia sh. bilion 621 na itakamilisha ifikapo Oktoba mwakani.
“Utekelezaji wa ujenzi katika majengo haya ni kati ya asilimia 28 na 55 na kazi zinaendelea pamoja na upandaji wa miti, ambapo Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) wanapanda miti 500,000 ili kuweka mandhari mazuri ya ofisi za umma.
SENSA YA WATU NA MAKAZI
Msemaji huyo alisema maandalizi ya Sensa ya watu na Makazi yamefikia asilimia 88 na kazi ya utengaji wa maeneo ya kuhesabia watu na majengo kwa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar imekamilika kwa asilimia 100.
Amesema kazi kubwa inayoendelea sasa ni kutoa elimu na kuhamasisha watu kujiandaa kuhesabiwa.
Msemaji huyo alisema maandalizi yamefikia asilimia 88 na kazi ya utengaji wa maeneo ya kuhesabia watu na majengo kwa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar imekamilika kwa asilimia 100.
Alisema kazi kubwa inayoendelea sasa ni kutoa elimu na kuhamasisha watu kujiandaa kuhesabiwa.
ANWANI ZA MAKAZI
Msigwa alisema utekelezaji wa operesheni ya anwani za makazi umefikia asilimia 95, ambapo makazi zaidi ya milioni 12.3 yamepata anwani, ikiwa ni zaidi ya makadirio yaliyowekwa ya kutoa anwani za makazi milioni 11.7.
Amesema utoaji wa anwani za makazi utabaki kuwa endelevu hata baada ya muda wa operesheni kumalizika kwa sababu nyumba zinaendelea kujengwa.
“Sasa ni kweli uwekaji wa vibao kwenye nyumba na mitaa unaendelea katika maeneo mbalimbali kwa mujibu wa sheria kila mwananchi anatakiwa agharamie yeye mwenyewe kukiweka na viongozi katika maeneo mbalimbali wamekubaliana na wananchi jinsi ya kutekeleza jambo hili,” alisema.
Na FRED ALFRED, DODOMA