HUENDA tunalifahamu Soko Kuu la Kariakoo, lakini tusijue undani wake, mbali na kuwa kitovu cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki, soko hilo lina historia nyingine za kusisimua.
Umaarufu wake unatokana na umri wake ambapo hadi mwaka huu linatimiza miaka 46, tangu lijengwe rasmi Disemba 8, mwaka 1975, lakini huo haukuwa mwanzo wa kutumika kwake.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, Soko la Kariakoo linakadiriwa kuwa na wafanyabiashara 1,662 waliopanga bidhaa zao katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya soko.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Wamachinga Tanzania, Steven Lusinde, anasema takribani watu 8,000 hadi 10,000 kutoka ndani na nje ya Tanzania wanahudumiwa katika soko hilo kwa siku wakifuata bidhaa mbalimbali.
Historia ya ujenzi hadi kuungua kwake
Ni ngumu kueleza fahari ya soko hilo bila kumtaja Mtanzania Arch Beda Amuli, ambaye ndiye msanifu wa jengo la soko hilo, aliyebuni na kuchora ramani yake.
Kwa mujibu wa Jarida la nani ni nani Tanzania ‘Who’s who in Tanzania’, Mhandisi Amuli alizaliwa Mei 27, mwaka 1938, Masasi mkoani Mtwara.
Alisoma katika Shule ya Saint Andrew’s ambayo sasa inafahamika kwa jina la Shule ya Sekondari Minaki na baadaye kujiunga na Chuo cha Royal cha Afrika Mashariki kilichopo Nairobi nchini Kenya.
Arch Amuli alijiunga na Taasisi ya Teknolojia ya Israel na ndiye mwanafunzi wa kwanza wa Afrika kuwa na shahada ya juu ya usanifu majengo aliyoipata mwaka 1964.
Hadi soko hilo linawaka moto Julai 10, mwaka huu ilikuwa ni siku ya maadhimisho ya miaka mitano ya kifo chake kilichotokea siku na mwezi kama huo lakini mwaka 2016.
Udadisi wa gazeti hili, umebaini kuwa Arch Amuli mbali na Soko la Kariakoo amesimamia ujenzi wa miradi mingine mikubwa na ya historia nchini.
Taarifa za kina za kesi ya madai kashfa Na 29/2008 aliyoifungua Arch Amuli dhidi ya aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Kariakoo Kuboja Ng’ungu, Mhariri wa Gazeti la Mtanzania na Kampuni ya Habari Coporation baada ya kuchafuliwa jina lake kwa kudaiwa hakusomea kazi ya usanifu zifafanua shughuli alizozifanya nchini.
Kwa mujibu wa aliyekuwa Jaji wa Kesi hiyo, Profesa Ibrahim Juma, vielelezo vilivyowasilishwa na Arch Amuli katika kesi yake hiyo, vilibainisha shughuli alizozifanya nchini tangu alipohitimu shahada ya juu ya usanifu majengo.
Anasema vielelezo hivyo vimeweka wazi kuwa Arch Amuli ndiye aliyesanifu na kusimamia ujenzi wa Hoteli ya Kilimanjaro ambayo sasa ni The Hayyat Regency Hotel, baada ya kujiunga na kampuni ya Zevet International Architect and Engineers of Tel Aviv ambayo ilishinda tenda ya kuchora mchoro wa ujenzi wa Hoteli hiyo.
Anabainisha baada ya kampuni hiyo kushinda tenda hiyo, ilimtuma Arch Amuli jijini Dar es Salaam kama mwakilishi wake ili kusimamia ujenzi wa jengo la hoteli hiyo.
Profesa Juma ambaye sasa ni Jaji Mkuu wa Tanzania, anaongeza kuwa vielelezo vya Arch Amuli vilieleza kuwa alifanya kazi na kampuni hiyo ya ZEVET kwa miaka mitano na baadaye kuhamia kampuni ya usanifu majengo ya BJ AMULI.
Anafafanua kuwa akiwa katika kampuni hiyo ndipo walipopata mradi wa ujenzi wa jengo la Soko la Kariakoo kati ya mwaka 1972 hadi 1974 na ndiye aliyechora mchoro wa jengo la Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Chuo cha Mafunzo cha Benki ya Taifa ya Biashara(NBC) ambacho kwa sasa ndicho Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa.
Chimbuko la Soko la Kariakoo
Historia ya jina Kariakoo na Soko la Kariakoo inaanzia enzi za Ukoloni wa Mjerumani wakati wa Tanganyika.
Mahala lilipo Soko la Kariakoo palijengwa jengo la utawala wa Wajerumani kwa ajili ya ukumbi wa kuadhimishwa na kutawazwa kwa Mfalme Kaiser Wilheim wa Ujerumani.
Lakini mara tu baada ya jengo kukamilika, Vita kuu ya Kwanza ya Dunia ilianza na Waingereza waliuteka mji wa Dar es Salaam na kulitumia jengo hilo kama kambi ya jeshi kwa askari waliojulikana kama “Carrier Corps” kwa jina la kigeni, yaani wabeba mizigo likitafsiriwa kwa Kiswahili.
Jina hilo la maaskari wabeba mizigo katika Kiswahili lilitamkwa “karia-koo” na liliendelea kutumika kama jina la eneo lote linalozunguka eneo lilipo jengo hilo la soko la Kariakoo.
Baada ya vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kuisha mwaka 1919 na nchi kuanza kutawaliwa na Waingereza, jengo hilo lilianza kutumika kama Soko na kuhudumia wakazi wa mji huu.
Wakati huo wafanyabiashara walikuwa wakiuza bidhaa zao sakafuni kwa sababu hapakuwa na meza. Wafanyabiashara waliendelea kufanya biashara sakafuni hadi miaka ya 1960 wakati meza za saruji zilipojengwa.
Kadri Jiji la Dar es Salaam lilivyokua na wakazi wake kuongezeka, ndivyo Soko lilivyokuwa likishindwa kumudu kutoa huduma nzuri kwa wananchi.
Pamoja na kubanana katika soko hilo na biashara kufanyika katika mazingira yasiyoridhisha, pia halikuwa na maghala ya kuhifadhia bidhaa. Hali hiyo iliwafanya viongozi wa Halmashauri ya Jiji kuona haja ya kuwa na soko kubwa na la kisasa kulingana na maendeleo ya Jiji na hivyo wakaanza kujadili uwezekano wa kujenga soko jipya.
Uamuzi wa kujenga Soko Kuu la Kariakoo la sasa, ulifanywa na Serikali mnamo mwaka 1970.
Serikali iliagiza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kujenga Soko jipya la kisasa ambalo lingechukua nafasi ya Soko la zamani na ujenzi ulianza rasmi mwezi Machi 1971.
Shughuli za ujenzi zilikamilika mwezi Novemba 1975, na lilifunguliwa rasmi 08/12/1975 na Rais Nyerere.
Na Juma Issihaka