MKUU wa Jeshi la Polisi Nchini, Inspekta Jenerali Simon Sirro, ameahidi kuendelea kupambana na wahalifu, huku akiwataka wazazi kutoa taarifa za watoto wao wanaowabaini kuwa na viashiria vya uhalifu.
Amesema Jeshi hilo, lina rekodi zote za wahalifu, hivyo hakuna mhalifu atakayetoroka au kufanya uhalifu, akabaki salama.
IGP Sirro alibainisha hayo, alipokuwa akihojiwa katika moja ya vituo vya televisheni nchini na kuongeza kuwa mwakani Jeshi hilo litaendeleza mapambano dhidi ya wahalifu, huku akionya hakuna atakayebaki salama.
“Mzazi ukimkumbatia mtoto mwenye viashiria vya uhalifu ni hatari sana…kwa mfano, mtoto wako hataki kusoma, anakuita kafiri usinyamaze toa taarifa kwa kuwa tutamchukua na kumfundisha,” alieleza.
Aidha, alisema Jeshi hilo limejiimarisha zaidi kupambana na uhalifu na wahalifu, hivyo mtu akitumia vibaya silaha kwa madai ya kukusanya fedha watapambana nao.
“Tunayo rekodi nzuri ya uhalifu, hivyo wahalifu waliokimbia tutashughulika nao na hakuna atakayebaki salama… kila mtu afuate sheria,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, IGP Sirro aliwataka Watanzania kutotumia vibaya mitandao ya kijamii, kwa kuwa atakayebainika atachukuliwa hatua stahiki.
“Msitumie mitandao kwa kuleta vurugu nchini, wizi kwasababu unapofanya uhalifu unanidhalilisha mimi na Jeshi, hivyo sitakubali…,” alionya.
Mbali na hayo, Sirro aliwahimiza Watanzania kuzingatia ulinzi shirikishi hususan maeneo ya mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma kwasababu wapo karibu na nchi ya Msumbiji ambayo haijatulia kiusalama.
Aliwasihi wakazi wa mikoa hiyo kutoa taarifa mapema pindi wanapobaini uwepo wa viashiria vya uhalifu, kabla havijaleta madhara.
Na ATHNATH MKIRAMWENI