Rais wa Marekani Joe Biden amesema Israel inaanza kupoteza uungwaji mkono kimataifa kutokana na “mashambulio ya kiholela ya mabomu” dhidi ya Gaza.
Kauli hiyo ya Bw Biden ya Jumanne ,alipokuwa akizungumza na wafadhili katika hafla ya kuchangisha pesa inaashiria ukosoaji wake mkubwa zaidi wa uongozi wa Israel’
Bw Biden amekuwa akitoa msaada kwa nchi hiyo tangu Hamas ilipoanzisha mashambulizi yake tarehe 7 Oktoba.
Huku akisisitiza kwamba Israel inaweza kutegemea uungwaji mkono wa Marekani, Biden alitoa onyo la moja kwa moja kwa serikali yake.
“Usalama wa Israel unaweza kuitegemea Marekani, lakini hivi sasa ina zaidi ya Marekani. Ina Umoja wa Ulaya, ina Ulaya, ina sehemu kubwa ya dunia,” aliwaambia wafadhili katika hafla ya kuchangisha pesa za kampeni yake ya kuwania tena urais mwaka 2024 iliyofanyika Washington.
“Lakini wanaanza kupoteza uungwaji mkono huo kwa kupiga mabomu kiholela ,” alisema.
Bw Biden, hata hivyo, aliongeza kuwa “hakuna hoja kuhusu kukabiliana na Hamas” na akaongeza kuwa Israeli ina “kila haki” kufanya hivyo.
Kiongozi huyo wa Marekani amekabiliwa na shinikizo linaloongezeka, ikiwa ni pamoja na kutoka ndani ya Chama chake cha Democratic, kumtaka kudhibiti kampeni ya kijeshi ya Israel.
Matamshi yake yanawiana na hatua zilizochukuliwa hivi karibuni za utawala wake kuhusu vita, huku maafisa wakiitaka Israel “kuweka kipaumbele kulinda maisha ya binadamu” na kutoa maelekezo ya wazi zaidi ili kuruhusu watu kuepuka vita.
Maafisa wakuu wa Marekani pia wameonyesha kutoridhika na kuongezeka kwa mashambulizi ya kijeshi ya Israel huko Gaza.
Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas mjini Gaza imesema zaidi ya watu 18,400 wameuawa kwa mashambulizi ya Israel tangu tarehe 7 Oktoba, wakati Hamas ilipoingia kwenye eneo lenye ulinzi mkali la Israel na kuwaua watu 1,200.
Katika taarifa yake ya Jumanne, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema Israel imepokea “uungwaji mkono kamili” wa Marekani katika vita vyake vya ardhini na katika lengo lake la kuiangamiza Hamas na kuwaokoa mateka.
Aliongeza kuwa Washington ilikuwa imezuia “shinikizo la kimataifa la kusitisha vita”.
“Ndiyo, kuna kutokubaliana kuhusu ‘siku iliyofuata baada ya Hamas’ [kufanya mashambulizi] na ninatumaini kwamba tutafikia [makubaliano] hapa pia,” alisema.