Na AMINA KASHEBA
MACHI 10, mwaka huu ilikuwa ni siku ya kipekee kwa nyota mpya wa muziki wa Bongo Fleva, Angelina George ‘Anjellah’.
Anjellah ni ingizo jipya katika muziki huo kupitia lebo ya Konde Gang inayomilikiwa na Rajabu Kahali ‘Harmonize’.
Msanii huyo aliyesota kupata ulaji kwa wasanii wakubwa wanaomiliki lebo zenye ushindani mkubwa nchini, hatimaye alikula shavu baada ya kuonwa na Harmonize akiwa mtaani akiimba kwa kurudia nyimbo za wasanii mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Ili kuonyesha kuwa Harmonize hakubahatisha kumpa nafasi Anjellah katika lebo yake, alimtambulisha kwa kuimba naye nyimbo ya ‘All Night’ ikiwa ni nyimbo yake ya kwanza kabla ya kumthibitisha katika lebo yake.
Hatimaye mwishoni mwa wiki iliyopita, lebo ya Konde Gang ilimkaribisha na kumtambulisha rasmi msanii huyo katika hafla iliyofanyika makao makuu ya studio za Harmonize.
Hapo ndipo safari rasmi ya Anjella ilipoanza, alipanda jukwaani kutumbuiza nyimbo mbalimbali za wasanii wengine kabla ya kuimba nyimbo yake mpya.
Huku akishangiliwa na mamia ya mashabiki waliojitokeza katika utambulisho huo, Anjella alitambulisha singo ya ‘Kama’.
Singo hiyo ya imekuja mwezi mmoja baada ya kutoka na kibao cha All Night alichoshirikiana na Harmonize.
Kuingia katika muziki kwa msanii huyo ni dhahiri kuwa kumezidi kuongeza ushindani wa wanawake katika muziki huo pendwa Afrika Mashariki na Kati.
Akizungumza baada ya kutambulishwa, Anjellah alisema moja ya malengo yake ni kuwa miongoni mwa wasanii bora wa kike wanaotambulika Afrika jamabo ambalo ni rahisi kulifikia baada ya kujiunga na lebo kubwa nchini.
“Nimehaingaika sana hadi kufikia hapa nilipo leo, namshukuru Mungu, uongozi nzima wa Konde Gang chini ya Harmonize, mashabiki na Watanzania wote mliokuwa mkinipa moyo kabla sijapata nafasi hii ya kipekee ambayo wanamuziki wengi walitamani kuipata”, alisema Anjellah.
Aliongeza kuwa baada ya kupata bahati ya kuwa msanii wa kwanza katika lebo hiyo, hatabweteka kwani atahakikisha anatunga na kuimba nyimbo ambazo zitazidi kumpandisha chati na kutoa upinzani kwa wasanii wenzakewa kike.
Aidha Anjellah alieleza kuwa ataongeza bidii na maombi ili kufanikisha ndoto zale nyingi na kupata mafanikio kama ambayo wasanii wenzake wa kike waliotangulia kwenye muziki wamepata.
Mwimbaji huyo anasema kwa sasa bidii zote anaziweka katika kazi na kusikiliza watu waliotangulia katika muziki ili kupata kitu cha utofauti katika muziki.
“Unajua jambo nzuri ni kusikiliza wakubwa wako walipoita wamefanya nini hadi kufikia hapo walipo kwani lengo langu nami ni kufika mbali ikiwemo kufanya kolabo na wasanii wakubwa ndani na nje ya nchi.
“Nitahakikisha naitumia vyema nafasi niliyopata, hii ni bahati ya kipekee sana, sitaichezea wala kumdharau aliyefanikisha ndoto zangu,” aliongeza.
Msanii huyo anaongeza kwa kusema kuwa atahakikisha anafanya kazi kwa bidii na kusikiliza ushauri ambao anaamini utamuongezea ufanisi katika kazi yake.
Akizungumzia changamoto ambazo amepitia hadi kufikia sasa, Anjellah anasema kuwa alikuwa akipigwa mara kwa mara na wazazi wake pindi alipotoroka nyumbani na kwenda mitaani kuimba.
Anasema kuwa kuna wakati wazazi wake walidhani kuwa anachelewa kurudi nyumbani kwa vile alikwenda kwa mwanaume wakati ukweli ni kuwa alikuwa akipita sehemu mbalimbali kuimba kwa ajili ya kutafuta ridhiki na si vinginevyo.
“Kila nilipochelewa kurudi nyumbani baba alinipiga na kunitolea maneno makali, nilivumilia huku nikiamini kuwa ipo siku wazazi wangu wataelewa kuwa nilikuwa nikitafuta nini,” alisema.
Anasema kuwa, hata Harmonize alipomtafuta na kutaka kumtoa kimuziki hakuamini kwani hakuwahi kufikiria kama msanii mkubwa kama huyo anaweza kumpa nafasi na kufanikisha ndoto zake kwani kuna idadi kubwa ya wasanii wenye uwezo ambao angeweza kuwasaidia lakini kumbe bahati ilikuwa yake.
Aliongeza kuwa huu ndio kwannza ameanza na atahakikisha hamuangushi Harmonize wala Watanzania ambao walikuwa nyuma yake katika kipindi ambacho alikuwa anatafuta nafasi ya kuonyesha kipaji chake.
Naye Harmonize alisema hajuti na hatajutia uamuzi wa kumuingiza Anjellah katika lebo yake kwani kipaji alichonacho ni kikubwa na kitaongeza ufanisi wa lebo yake.
Harmonize alisema kuwa baada ya miezi sita Anjellah atakuwa moto wa kuotea mbali na ametenga muda mwingi kwa ajili ya kumpika na kumshindanisha na wasanii wengine wa kike nchini.
“Baada ya muda mfupi Anjellah ndiye atakuwa msanii bora wa kike nchini, namuamini na nawahakikishia wapenzi wa muziki nchini kuwa binti huyu ni moto wa kuotea mbali,” alisisitiza Harmonize.