Na Happiness Mtweve, Mbeya
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) kikosi 844Kj Itende Mbeya kinazalisha gesi kwa kutumia kinyesi cha Ng’ombe na vyakula kwa ajili ya matumizi ya kupikia katika kikosi hicho.
Pia limepokea kilo 300 za mbegu za kahawa ambazo zitazalisha miche milioni moja kwa ajili ya kuigawa kwa wananchi huku mingine itatumika na kikosi hicho ikiwa ni mikakati ya kukuza zao hilo.
Akitoa maelezo kijana wa Jeshi wa kujitolea Damiani William kwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Charles Mbuge, wakati alipotembelea kikosi cha 844Kj Itende kwa ajili ya kukagua shughuli za kilimo mkakati.
William amesema uzalishaji huo wanaoufanya kwa kutumia mradi huu umeleta manufaa mengi katika kikosi hicho ambapo mchakato wa kuzalisha gesi hiyo unaanzia katika matanki mawili yenye uwezo wa kubebe lita 18000 kupitia katika chemba zinazopokea mchanganyiko huo kwa kutumia mabaki ya chakula kutengeneza gesi.
Amefafanua kuwa wanachanganya maharage ugali na kinyesi Cha Ng’ombe na kukipondapobda na baadaye inapatikana gesi ambayo wanaitumia kwa matumizi ya kupikia.
Mkuu wa JKT Meja Jenerali Mbunge amesema Jeshi hilo limejikita kuendeleza mazao ya biashara ya kimkakati yaliyotolewa maelekezo na Amiri jeshi Mkuu na Rais, Dk.John Magufuli ikiwemo zao la Kahawa.
Amefafanua kuwa mbegu hizo zimetolewa na Bodi ya Kahawa nchini ikiwa ni utekelezaji wa mkataba wa JKT na Bodi hiyo wa kuzalisha zao hilo.
Meja Jenerali Mbuge amesema katika kuhakikisha jeshi linajitegemea kwa chakula wamejipanga kuboresha mazao ya kimkakati likiwemo Hilo la Kahawa, mahindi, alzeti, Mpunga, korosho ili kusaidia kukuza uchumi wa taifa.
“JKT inatekeleza agizo la Rais Dk John Magufuli la kuwataka wajitegemee katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ili kuepuka kutegemea fedha za serikali,”amesema Meja Jenerali Mbuge.
Pia katika ziara hiyo mkuu wa JKT amezindua jengo la SGT Mess katika kikosi hicho lililogharimu kiasi Cha Tsh. milioni 90.