WILAYA ya Temeke, Dar es Salaam, imekamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ya sekondari 157, vilivyogharimu sh.bilioni 3.14 zilitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Makabidhiano ya vyumba hivyo yalifanyika katika Shule ya Sekondari Dovya iliyoko Chamazi wilayani Temeke ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya Jokate Mwegelo.
Akizungumza katika makabidhiano,Jokate amefafanua kwamba tayari vyumba vyote 157 vya madarasa ya sekondari katika Shule 25 vimekamilika vikiwa na meza na viti kwa wanafunzi kukalia
Jokate alimshukuru Rais Samia kuridhia wilaya hiyo kupewa sh.bilioni 3.14 za ujenzi wa madarasa hayo, ikiwa ni sehemu ya fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Alisema madarasa hayo mapya yataondoa adha ya wanafunzi waliochaguliwa kidato cha kwanza kuripoti kwa awamu na msongamano.
Pia alisema kutaboresha mazingira ya kufundisha, kujifunzia na matokeo yake ni kuimarisha ufaulu na kujikinga kikamilifu na mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19.
Jokate ameongeza kuwa “Tuna deni la kumlipa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha watoto wetu wanafanya vizuri katika masomo yao, fedha alizotupatia ni zaidi ya sh.bilioni tatu za ujenzi wa madarasa 157, hivyo tutakuwa tumezitendea haki kwa watoto wetu kufaulu,”
Jokate alisema wanafunzi watakaonufaika kuanzia mwaka huu ni milioni 12 na katika kipindi cha miaka mitano sh.trilioni 1.2 zitakazotolewa na Benki ya Dunia zitaboresha mazingira ya kusomea.



























