Na ASHURA ASSAD
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema kuna ongezeko kubwa la joto katika baadhi ya maeneo nchini, huku wataalamu wa afya wakitoa njia za kuweza kukabiliana nalo ili kujilinda kiafya.
Miongoni mwa njia za kukabiliana na hali hiyo ili kujilinda dhidi ya madhara mbalimbali, ikiwamo maradhi kwa kunywa maji mengi, kuepuka kuvaa nguo za kubana, hususan za ndani kwa wanaume, kuepuka matembezi yasiyo ya lazima juani na kujilinda na magonjwa ya mkojo.
Akizungumza na gazeti hili, Mchambuzi wa Hali ya Hewa kutoka TMA, Rose Senyagwa, alisema kuanzia Machi 11, mwaka huu, kiwango cha joto katika baadhi ya maeneo kiliongezeka kutoka nyuzijoto 32.2, zilizokuiwapo kabla ya hapo hadi 34.9, ikiwa ni ongezeko la juzi joto 2.7.
Alisema miongoni mwa maeneo yaliyoathirika na hali hiyo ni Pwani ya Kaskazini na Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Mchambuzi huyo, alisema kwa upande wa ukanda wa Kaskazini, Machi 12, mwaka huu, kiwango cha joto kiliongezeka kutoka nyuzijoto 32.5 hadi nyuzijoto 35.5, ikiwa ni wastani wa ongezeko la nyuzijoto tatu.
Hata hivyo, alisema hali ya unyevunyevu katika anga ya mwambao wa Pwani, imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 80, hivyo kusababisha fukuto kubwa kwa maeneo ya Pwani ya Bahari ya Hindi.
“Hali hi inatarajiwa kuendelea kwa muda wa wiki mbili kwenye mwezi huu wa Machi, katika maeneo ya ukanda wa Pwani na mvua za msimu wa Masika zinatarajiwa kunyesha baada ya kipindi hiki kupita,” alisema.
WATAALAMU WA AFYA WAZUNGUMZA
Katika hatua nyingine, wataalamu wa afya wamewataka wananchi kuchukua tahadhari mbalimbali katika kipindi hiki cha kuongezeka kwa joto, kwa lengo la kuepukana na madhara mbalimbali yanayoweza kusababishwa na hali hiyo.
Mtaalamu wa magonjwa ya ngozi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Dk. Elias Mwano, alisema katika kipindi hiki cha joto, mavazi ya kubana hayashauriwi kwani yanasababisha hewa kutopita vizuri kuingia mwilini.
Alisema wenye kupendelea kuvaa suruali za kubana, wanashauriwa kuziweka pembeni katika kipindi hiki cha joto kwani zinaweza kuwaletea madhara katika ngozi.
Madhara hayo ni pamoja na kuharibika kwa ngozi na wakati mwingine kusababisha tatizo la saratani.
“Kuna vijana ambao wamezoea kuvaa suruali za kubana na boksa (nguo za ndani) za kubana, wanatakiwa kuziweka pembeni kipindi hiki kwani zinaweza kufanya sehemu nyeti kushindwa kupata hewa na hivyo kutengeneza uwezekano wa kusababisha madhara,” alisema.
Alisema kipindi hiki inashauriwa kuvaa mavazi mepesi, ambayo yanapitisha hewa katika sehemu zote za mwili.
Aidha, alisema ni vyema pia kuepuka kupigwa na jua kwa muda mrefu, kwani kunaweza kuasababisha madhara katika ngozi na wakati mwingine kusababisha saratani, hususan kwa wale wenye kupendelea kutumia vipodozi vyenye viambata vya sumu.
Alisema katika kipindi kama hiki, inashauriwa wavae miwani au kujifunika miavuli ili kujikinga na miale ya jua, ambayo inaweza kuwasababishia matatizo ya macho.
Kwa upande wake, Dk. Julius Mwambapa kutoka Kituo cha Afya Mbagala, alisema inashauriwa kupunguza mizunguko isiyokuwa ya lazima ili kuepuka jua kali linalosababisha kupoteza nguvu mwilini.
Dk. Julius, alisema katika kipindi kama hiki, ndipo mlipuko wa magonjwa ya fangasi na mkojo hutokea, hivyo ni vyema kuzingatia ushauri wa madaktari na wataalamu wa afya.
Alishauri kunywa maji kwa wingi kulingana na maelekezo yanayotolewa kutokana na uzito wa mtu husika, na kwa wale ambao hawawezi kunywa maji mengi, wajitahidi kula matunda yenye asili ya maji kama mananasi na matikiti.
Dk. Raymond Mgeni kutoka Hospitali ya Rufaa Mbeya, alisema katika kipindi kama hiki, wazazi wanashauriwa kuchukua tahadhari kwa watoto, ikiwamo kuwanyonyesha kwa wingi wale ambao bado wananyonya.
Alisema wanatakiwa kuwanyonyesha kwa muda mrefu kwa sababu watoto wanapoteza maji mwilini kipindi hiki cha joto kali na maziwa ya mama huongeza maji kwa watoto.
Pia, aliwataka wazazi kuacha kuzunguka na watoto wadogo bila sababu ya msingi, kwani wanaweza kuhatarisha afya zao.
Mfanyabiashara wa vinywaji eneo la Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, Hassan Jumbo, alisema hali ya joto kwa upande wake imemuingizia faida katika biashara yake.
“Nisiseme uongo, kwa sasa biashara imekuwa nzuri kwa sababu watu wanakunywa sana maji, kwa kiasi chake imenisaidia sana,”alisema.