JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dodoma, imetoa tamko la kuwalaani baadhi ya wanaCCM, wanaopanga mbinu na mikakati ya kugombea urais mwaka 2025 na kusababisha makundi na migogoro ndani ya Chama.
Pia, imetoa pongezi kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa na maono makubwa kwa maendeleo ya Taifa.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa jumuiya hiyo mkoani Dodoma, Dk. Damas Mkasa, alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi za CCM mkoani humo.
Alisema wanaofikiria kuanzisha makundi ya uchaguzi wa urais mwaka 2025 ndani ya CCM siyo watu sahihi na hawakitakii mema Chama.
Dk.Mkasa alisema kupitia jumuiya anayoiongoza, wanalaani vikali makundi ya baadhi ya watu wachache wanaowaza uchaguzi wa urais mwaka 2025, badala ya maendeleo ya watu na vitu.
“Kati ya mashati ya kijani ambayo yatapambana kuhakikisha wanamuunga mkono Mwenyekiti CCM taifa na rais wa sasa ni pamoja na jumuiya ya wazazi mkoa wa Dodoma, ukiondoa wachache ambao wamechanganyikiwa kwa kuwa na uchu wa madaraka,”alisema.
Alisema Dodoma ndiyo ngome ya chama, hivyo Jumuiya ya Wazazi mkoa wa Dodoma haiwezi kuwavumilia watu wachache ambao hawajitambui licha ya kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Dk.Mkasa alisema Jumuiya ya wazazi na wanaCCM wanaendelea kumuunga mkono Rais Samia kwa kuwa kiongozi mwenye maono makubwa kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
“Nataka kuwaambia ndugu zangu wana CCM tuache unafiki, uzandiki, majungu na ninaweza kusema watu wa aina hiyo ni sawa na wachawi ndani ya chama,”alisema.
Alisisitiza kuwa Jumuiya itaendelea kumuunga mkono Rais Samia kwa kuwa baada ya muda mfupi amefanya mambo mengi ya maendeleo, hususan miradi iliyotokana na fedha za mkopo wa mashariti nafuu ya Uviko-19.
Tamko la Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Dodoma limekuja Kufuatia hotuba aliyoitoa Rais Samia Suluhu Hasan kukemea makundi ndani ya chama na kuwashangaa wanaobeza mikopo na tozo.
Na Happiness Mtweve, Dodoma