KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM, imempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kutimiza mwaka mmoja tangu aingie madarakani, ambapo amelinda tunu za taifa ikiwemo amani umoja na utulivu.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa NEC ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, ilisema Kamati Kuu ilikutana katika kikao maalumu, Ikulu ya Chamwino, Jijini Dodoma chini ya Mwenyekiti wa CCM Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo pamoja na mambo mengine ilimpongeza Rais Dk. Mwinyi.
“Kamati Kuu imempongeza Mheshimiwa Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kutimiza mwaka mmoja tangu kuingia madarakani kuwa Rais wa nane wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na kuendeleza mshikamano, kulinda tunu ya umoja, amani, utulivu sambamba na utekelezaji makini na imara wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025,” ilisema sehemu ya taarifa ya Shaka kwa umma.
Shaka alisema Kamati Kuu imeridhishwa na namna Rais Dk. Mwinyi alivyotekeleza Ilani ya Uchaguzi katika kipindi hicho na kufanikisha kuendeleza tunu ya umoja, amani na utulivu.
Pia, alisema Kamati Kuu ilimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ya ujenzi wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Mbali na hilo, alieleza kuwa, Kamati Kuu imefanya uteuzi wa Emmanuel Lekishon Shangai, kuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM Jimbo la Ngorongoro mkoani Arusha.
Uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo hilo utarajiwa kufanyika Desemba 11, mwaka huu, kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wake, marehemu William Tate Ole Nasha.
Aidha, Kamati Kuu imewateua Gulamhafeez Abubakar Mukadam na Ella’s Ramadhani Masumbuko kugombea kiti cha umeya katika Manispaa ya Shinyanga Mjini, mkoani Shinyanga.
Na MWANDISHI WETU, DODOMA



























