KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Mstaafu, Ngemela Lubinga, amesema watumishi wa umma kuwajibika kuwatumikia wananchi, si ombi, isipokuwa ni lazima.r
Hayo aliyasema kwa nyakati tofauti, akiwa katika ziara ya kikazi katika Wilaya za Liwale, mkoani Lindi, Tandahimba, Mtwara na Nyasa, Mkoa wa Ruvuma.
Alisema maendeleo ya haraka na yenye faida kwa Mtanzania, yatapatikana kwa kila mtu kuwajibika kikamilifu katika eneo lake la kazi, wakiwemo watumishi wa umma.
Kuhusu utekelezaji wa ilani ya CCM ya 2020-2025, Lubinga alisema mabilioni ya fedha yanayopelekwa wilayani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zisipofanyiwa ubadhirifu, maendeleo makubwa yatapatikana nchini kwa kipindi kifupi.
Kanali mstaafu Lubinga, alionyesha kukerwa na tabia ya baadhi ya viongozi na watendaji katika utumishi wa umma, kukwapua fedha za umma kwa masilahi binafsi, huku wananchi wakitaabika kwa kukosa huduma nzuri; zikiwemo za afya, maji na elimu.
Alitaka hatua kali za kisheria kuchukuliwa mara moja dhidi ya mtumishi yoyote wa umma atakayebainika kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.
“Mkuu wa wilaya, TAKUKURU mnafahamu serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, inatoa fedha nyingi sana kwa ajili ya miradi ya maendeleo, nawaagiza kuzisimamia ili zilete matokeo yanayotarajiwa,” alibainisha Kanali mstaafu Lubinga.
Alisema kwamba kwa waumini wa dini, mtumishi wa umma kutokuwajibika kulingana na vigezo vya ajira yake ni dhambi.
“Wewe usidhani dhambi ni kutamani tu mke wa mtu, tena hiyo inaweza kuwa na madhara kwa wachache, hebu fikiria daktari asipowajika, mwalimu asipowajibika, nesi asipowajibika, ndege ipo angani halafu rubani hawajibiki, si watu watakufa!,” alisema
Aliongeza kuwa: “Watumishi wa umma kuwajibika ipasavyo ni lazima na siyo ombi, si wewe mwenyewe uliandika barua ya maombi ya kazi na kuandika wako mtiifu, sasa wajibika.”
Kwa kuwa wilaya hizo zinapakana na nchi jirani, aliwataka wananchi kuepuka kuishi na watu ambao hawana uhakika na taarifa zao.
Kanali mstaafu Lubinga aliagiza kila balozi wa shina la CCM kuwa na kitabu cha wageni kwa ajili ya kuwasajili wanaongia na kutoka katika maeneo yao.
Alifafanua kwamba, amani na usalama, ni hali ambayo kila Mtanzania anapaswa kuitunza.
Alisema ni katika hali ya amani na usalama, shughuli za kujiletea maendeleo zinaweza kufanyika.
Kanali mstaafu Lubinga, alikuwa ziarani katika wilaya hizo kuanzia Septemba 15 hadi 20, mwaka huu;. kukagua uhai wa CCM katika ngazi ya shina, utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM na kuhimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika sensa mwakani.r
NA JACQUELINE LIANA, NYASA