MSANII mchekeshaji kutoka Uganda, Anna Kansiime, anatarajia kutoa burudani ya ‘Stand Up Comendy’ Desemba 4 mwaka huu, katika Viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam.
Shoo hiyo iliyopewa jina la ‘December to Remember’ itashirikisha wachekeshaji mbalimbali wa Tanzania.
Akizungumza Dar es Salaam, Muandaji wa burudani hiyo, Zamaradi Mketema amesema lengo ni kufurahi na kujipongeza katika kumaliza mwaka vizuri.
Zamaradi ameeleza kuwa burudani hiyo itakuwa endelevu ili kubadilisha mawazo na kupata marafiki wapya katika tukio hilo.
“Tukio hili litaacha historia, pia tunaanza na Kansiime ila mwakani kutakuwa na msanii mkubwa zaidi yote ni kufurahi na kubadilishana mawazo, ” amesema.
Muandaji huyo amefafanua kuwa burudani hiyo inaruhusiwa kuja na mtu wa rika lolote kutokana na maudhui ya uchekeshaji.
“Hili tukio litakuwa kubwa unaruhusiwa kuja na mtu yoyote yule pia tumeona kufanya jambo hili kutokana kuna baadhi ya kundi wanatamani kwenda mahali kupumzisha akili, huu ndiyo muda wao.” amesema.
Zamaradi alitaja baadhi ya wachekeshaji ambao watakuwepo katika tukio hilo ni Emmanuel Matias ‘Mc Pilipili’ na Mpoki huku zikisindikinzwa na burudani mbalimbali.
Na AMINA KASHEBA