BAADHI ya wananchi wa Wilaya za Bukoba, Muleba na Karagwe mkoani Kagera wamepongeza juhudi za serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuongeza vituo vya kutolea huduma ya chanjo ya corona kutoka 18 hadi 284.
Wakizungumza na UhuruOnline, wananchi hao wamesema walikuwa na hamu ya kupata chanjo hiyo ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo, lakini changamoto ilikuwa ni umbali mrefu na jiografia ya maeneo yao ilivyokaa mpaka wafike katika vituo vya kutolea huduma hiyo.
Mkazi wa Kisiwa cha Goziba kilichopo ndani ya Ziwa Victoria, Wilaya ya Muleba, Joseph Kazimoto (67) amesema wamekuwa wakisikia viongozi wakilalamika mwitikio wa wananchi kupata chanjo hiyo ni mdogo, lakini wakasahau kuwa vituo vilikuwa mbali na makazi ya wananchi wao.
“Nina makazi sehemu mbili majini (kisiwani) na nchi kavu, lakini ukiangalia pale walipoweka kituo cha kutolea chanjo ni umbali wa kilometa kati ya 30 hadi 35 kutoka kisiwani kwenda kituo cha afya Kaigara, unasafiri kwa mtumbwi nauli sh. 10,000 wakati mwingine kunakuwepo upepo mkali ziwani, hivyo tunakosa huduma hiyo kutokana na mazingira,”alisema Kazimoto.
Amesema alisikia kwenye vyombo vya habari kuwa huduma ya chanjo imeboreshwa ambapo kwa sasa serikali imeamua kuanzisha mpango shirikishi na harakishi wa kuhakikisha wananchi wanafikiwa katika maeneo yao na kupatiwa chanjo bila gharama yoyote.
Alieleza yeye na jamii inayomzunguka wameona mpango huo ni njia bora ya kutatua changamoto ya kukosa chanjo, hivyo kupongeza jitihada hizo.
Wajasiriamali wanaoishi katika Kisiwa cha Musira km 15 kutoka Manispaa ya Bukoba, Salome Nyamwiza na Rachal Mwita walisema diwani wa kata yao ya Miembeni, Richad Mwemezi, alipita mara nyingi akiwahamasisha wajitokeze kupata chanjo kwa kuwa ni bure, kinga na haina madhara.
“Uhamasishaji umefanyika sana, lakini changamoto ilikuwa ni maeneo ya kupata huduma na kuna wakati alikuja Mkuu wa Wilaya ya Bukoba aliyestaafu Deodatus Kinawiro tulimuomba tuletewe huduma ya chanjo ya mkoba kama wanavyofanya kwa kliniki za wajawazito na watoto maana kila Alhamisi wanakuja huku wahudumu kutoa huduma,” alisema Salome.
Aliongeza kuwa: “Naona serikali imesikia kilio chetu na kuamua kuongeza vituo vya kutolea huduma hivyo nina amini katika kisiwa chetu tutapata kituo.”
Mkazi wa Kijiji cha Ruhita kilichopo wilayani Karagwe, Siima Silvery, alisema ili mtu apate chanjo alililazimika kusafiri kwa pikipiki kwa gharama ya sh. 6,000 kwenda kupata huduma katika Hospitali Teule ya Nyakahanga hali hiyo iliwakatisha wengi tamaa hasa wale wenye kipato cha chini.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Issesanda Kaniki, alisema kupitia Wizara za Afya, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na wadau wa afya walibaini kuwa mwitikio mkubwa wa watu kupata chanjo uko chini ndipo wakaamua kufuatilia na kutafuta chanzo.
“Kwa Kagera mwanzo wakati chanjo imeanza kutolewa tulikuwa na vituo 18 tu mkoa mzima, tukaongeza vikawa 27, vikaongezeka na kuwa 81, lakini bado vikaonekana havitoshi na sasa tumeongeza mpaka 284 kati ya vituo 334 vya kutolea huduma za afya
“Tayari tumeshapeleka chanjo za kutosha na watu wameanza kuchanja hivyo nawaomba wananchi wajitojeze wapate huduma hiyo kuanzia umri wa miaka 18 na yale maeneo ambayo hayafikiki kirahisi tumeandaa chanjo tembezi,” alisema.
Aliwaeleza wananchi wenye wasiwasi juu ya chanjo hiyo kuwa ni salama haina madhara yoyote huku ndani ya kipindi kifupi zaidi ya watu 15,000 wamechanjwa mkoa mzima.
Na ANGELA SEBASTIAN, BUKOBA





























