Na NASRA KITANA
WADAU wa soka nchini, wamezichambua timu zitakazoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho msimu ujao na kuzitaka kufanya maandalizi ya mapema.
Mchambuzi Alex Kashasha, amesema kuwa hiyo ni nafasi nzuri kwa Taifa lakini timu ambazo zitapata ushiriki, zinatakiwa kufanya maandalizi ya mapema kwani hiyo ni nafasi yao ya kuonyesha kiwango walichokuwa na wachezaji kujiuza Afrika.
“Nafasi hii itatuletea faida kubwa katika nchi, hasa katika soka kwani tutaweza kujitangaza lakini pia vijana wetu watapata nafasi ya kuonekana na wakionyesha juhudi basi watapata nafasi ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi,” amesema Kashasha.
Ali Mayai, amesema nchi imepata nafasi ya kuwakilishwa na timu nne, hivyo ni fursa kwa timu zitakazoshiriki kuanza kufanya maandalizi mapema.
Mayai amesema timu zitakazopata nafasi ya kuiwakilisha nchi kimataifa, zinatakiwa kufanya usajili wa hali ya juu ili kuhakikisha zinafanya vyema na kufika mbali zaidi msimu ujao.
“Timu zifanye maandalizi ya mapema na kuhakikisha zinasajili wachezaji wenye kiwango bora, tofauti na hapo tutakuwa tunasindikiza wenzetu kila msimu,” amesema Mayai.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF), jana Juni 21, limethibitisha Tanzania kuingiza timu nne katika mashindano hayo kwa msimu wa mwaka 2021/2022.
KAULI YA TFF
Akizungumza Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo, amesema timu mbili zitashiriki katika Ligi ya Mabingwa na nyingine mbili zitashiriki Kombe la Shirikisho msimu ujao.
Ndimbo amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi 12 ambazo zitaingiza timu nne kwa msimu wa 2021/2022 , huku timu mbili zikiwa zinacheza Ligi ya Mabingwa Afrika na timu mbili zingine zitacheza Kombe la Shirikisho Afrika.
Hatua ya raundi ya awali itachezwa kati ya Septemba 10-12, mwaka huu na marudiano kati ya Septemba 17-19, mwaka huu.
Upande wa hatua ya makundi katika mashindano hayo itachezwa kati ya Februari 11-13, mwakani na upande wa timu ambazo zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ni zile ambazo zitamaliza nafasi mbili za juu, huku upande wa shirikisho Afrika akienda bingwa wa Kombe la FA na mshindi wa tatu katika ligi.
Hadi sasa, nafasi ya kwanza mpaka tatu katika Ligi Kuu zinashikiliwa na Simba, Yanga na Azam huku upande wa FA, hatua ya nusu fainali tayari zimeingia timu za Biashara United, Yanga, Azam na Simba.
Hii ni mara ya pili Tanzania kupata bahati ya kuingiza timu nne baada ya msimu wa mwaka 2019/2020, lakini timu zote ziliishia hatua za awali.