MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba, amehimiza wazee wa mkoa huo kupuuza maneno ya upotoshaji dhidi ya chanjo ya UVIKO19, badala yake wakachanjwe ili kunusuru afya zao.
Amesema wazee ni moja ya makundi yaliyopewa kipaumbele na kuwataka waangalie afya zao na ustawi wa maisha yao, badala ya kusikiliza taarifa za wapotoshaji.
Kate amesema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani, yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
Amesema kuna baadhi ya watu walioshiba, wanatoa taarifa za uongo na hawana nia njema na huruma na kundi hilo muhimu.
“Baadhi ya wazee wako mahututi kwa sababu hawakuchanja, nawaomba sana wazee wa mkoa wa Dar es Salaam mkachanje,chanjo zipo, achaneni na porojo na propaganda, kuna watu wao wameshiba wanataka wazee tufe naombeni mkachanje,” amesema.
Kwa mujibu wa Kate, Chama kinatarajia kuwafikia wazee walipo ili kiwapatie elimu na kuwahimiza dhidi ya chanjo hizo.
“Kama Chama tutakuja huko huko kuwahimiza, nawasihi wazee wenzangu tukachanje kwa faida ya afya zetu, tusicheze na maisha,”alisema.
Hata hivyo, Kate alimwagiza Mwenyekiti wa Wazee Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Matimbwa, kuwahimiza wenzake kuhusu umuhimu wa chanjo hizo.
Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya za mkoa huo, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Nyangasa, alisema wapo tayari na wamejipanga kuhakikisha wazee wanapata huduma zote stahiki na kuangaliwa kwa jicho la pekee.
“Sisi wakuu wa wilaya,tutahakikisha kundi hili muhimu linaaangaliwa kwa jicho la pekee na kupata huduma zote katika nchi yetu,”alisema.
Fatma alisema kwa sasa kuna mikakati mbalimbali inaendelea, ikiwemo utolewaji wa vitambulisho vya kuwasaidia kupata huduma za afya.
Alisema serikali imeweka mikakati mbambali ya kuhakikisha wazee wanapata elimu ya kutosha juu ya matumizi ya vitambulisho hivyo.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni matumizi sahihi ya kidigitali kwa ustawi wa rika zote.
IRENE MWASOMOLA Na SAMIRA OMARY(tudarco)



























