Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa
MAHAKAMA ya Wilaya ya Maswa, Mkoa wa Simiyu, imemhukumu, Katibu wa Baraza la Kata ya Binza, Daud Elias, kulipa faini ya sh. 500,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela, baada ya kupatikana na hatia ya kuomba rushwa ya sh 50,000.
Hukumu hiyo ilitowlewa mwishoni mwa wiki na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Enos Misana, baada ya mshitakiwa kukiri kosa lake.
Awali, Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Carson Nkya, aliieleza mahakama hiyo kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo, Juni 6, mwaka huu na kufunguliwa kesi ya jinai namba 38/2021.
Alidai mshitakiwa akiwa Katibu wa Baraza la Kata hiyo aliomba kiasi hicho cha fedha kwa Mussa Jigeleka ili amwandikie hukumu yenye upendeleo katika shauri la madai lililokuwa linamkabili katika baraza hilo.
Mwendesha mashitaka huyo alidai mshitakiwa awali aliomba rushwa y ash. 70,000 lakini baadae walikubaliana atoe sh. 50,000.
Alidai baada ya TAKUKURU kupata taarifa hizo, walitengeneza mtego ambao walifanikiwa kumkamata mjumbe wa baraza la kata hiyo, Emanuel Gibe ambaye alitumwa kupokea fedha hizo.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Nkya alisema kosa alilofanya mshitakiwa ni kinyume cha kifungu cha 15 cha sheria ya TAKUKURU namba 11 ya mwaka 2017.



























