Na AMINA KASHEBA
MPINZANI wa bondia Twaha Kiduku, Tshibangu Kayembe, amewasili nchini na kutamba kumchakaza mpinzani wake.
Kayembe, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), atapanda ulingoni kuzichapa na Kiduku katika pambano la raundi 10 uzani wa Middle Weight.
Pambano hilo litafanyika keshokutwa katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.
Akizungumza jana, Kayembe alisema licha ya kuwa mpinzani wake ana rekodi nzuri, atahakikisha anaivuruga kwa kushinda pambano lao katika raundi za awali.Kayembe alisema amefanya maandalizi makali chini ya wakufunzi tofauti na yupo tayari kuzichapa na Kiduku.
“Nipo fiti na nina uhakika wa kufanya vizuri licha ya kuwa pambano litakuwa gumu, najua Kiduku ni mjanja na huwa hakubali kupoteza kirahisi lakini nitahidi kumdunda kwa pointi,” alitamba Kayembe.
Alipoulizwa kuhusu maandalizi yake, Kiduku alisema amemuacha Kayembe atambe lakini kabla ya raundi ya tano atakuwa amekwishatangaza ubingwa.
Kiduku alisema hatapoteza pambano lolote litakalofanyika nchini na kumtaka mpinzani wake kujiandaa kwa kichapo.
Mratibu wa pambano, Ernest Mopao, alisema maandalizi yamekamilina na kesho mabondia watapima uzito na afya.
Licha ya pambano la Kiduku na Kayembe, kutakuwa na pambano lingine litakalowakutanisha Yonas Segu wa Tanzania na Mmalawi, Hannock Phiri.