Na REHEMA MOHAMED
KESI inayomkabili mchekeshaji Idrisa Sultan na wenzake, imeshindwa kuendelea na usikilizwaji kutokana na hakimu anayeisikiliza kuwa na majukumu mengine.
Washitakiwa hao wamepanda kizimbani leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, ambapo Wakili wa Serikali, Neema Mushi, alidai Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Luboroga, anayesikiliza shauri hilo ana majukumu mengine.
Kutokana na hali hiyo, Wakili Neema aliiomba mahakama iahirishe usikilizwaji wa kesi hiyo hadi tarehe nyingine. Hakimu Simba aliahirisha usikilizwaji huo hadi Julai 5, mwaka huu.
Mbali na Idrisa, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Isihaka Mwinyimvua na Doctor Ulimwengu, ambao kwa pamoja wanakabiliwa na kosa la kurusha maudhui mtandaoni, bila ya kuwa na leseni.
Washitakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo, kati ya Machi 8, mwaka 2016 na mwaka 2020, maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa wanadaiwa kurusha maudhui hayo kupitia televisheni mtandaoni katika akaunti ijulikanayo kama Loko Motion, bila ya kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).