BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Twaha Kiduku ameanza kambi Ifakara, Mkoani Morogoro, ili kujiandaa na pambano dhidi ya mpinzani wake Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’.
Pambano hilo linatarajiwa kufanyika Agosti 20, mwaka huu, katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na UhuruOnline, Twaha Kiduku amesema ameanza kambi mapema ili kupata mafunzo makali ambayo yatamuweka fit kwa pambano hilo la kisasi.
Kiduku ameeleza kuwa mchezo wa ndondi ni kazi yake, hivyo wajibu wa kujiandaa na kuweka mambo sawa ili kuwapa burudani nzuri mashabiki zake.
“Ngumi ndiyo ajira yangu ambayo inaendesha maisha yangu, ninapaswa kuweka mazingira mazuri kama wavyofanya watu wengine katika kazi zao,” amesema Kiduku.
Bondia huyo amesema katika kujifua huko, Mbunge wa Morogoro mjini, Aziz Abood, amekuwa mstari wa mbele kuisimamia kambi yake.
“Namshukuru Mbuge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Aziz Abood kusimamia kambi yangu, nitafanya vizuri katika pambano langu na mapambano mengine yajayo,” amesema Kiduku.
Kiduku amewaomba Watanzania na mashabiki wake kujitokeza kwa wingi katika pambano hilo ili kumpa hamasa ya kushinda.
Ikumbukwe kuwa, pambano la awali Kiduku alishinda kwa pointi, pambano lililofanyika katika uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam mwaka jana.
Na Amina Kasheba