MABONDIA Twaha Kassim ‘Twaha Kiduku’ na Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’ kesho wanatarajia kupima uzito na afya katika ukubwa Ubungo Plaza, kuelekea katika pambano la marudiano la ‘Usiku wa Deni’.
Pambano hilo litafanyika katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam kwa ajili ya kuondoa ubishi nani mbabe zaidi ya mwenzake.
Akizungumza kwa simu na UhuruOnline, Kiduku amesema maandalizi ni mazuri, amejipanga kuonyesha burudani ya kipekee.
Kiduku amesema mchezo wa ndondi ni kazi yake, hivyo atahakikisha anaonyesha uwezo mkubwa kwa mashabiki wake.
“Nawaomba mashabiki zangu wajitokeze katika tukio la kupima uzito, nimejipanga vizuri nashukuru wakazi wa Morogoro na vitongoji vyake kwa kunisapoti,” amesema Kiduku.
Hapo awali Kiduku alishinda kwa pointi baada ya kumchakaza mpinzani wake, Dullah Mbabe pambano lililofanyika katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Septemba mwaka jana.
Mratibu wa pambano hilo, Kapteni Selemani Semunyu amesema amefurahi kuona malengo yake yametimia katika upande wa zawadi.
Semunyu amesema, hapo awali alitamani kuweka thamani kubwa ya zawadi ambayo itawapa moyo mabondia kufanya vizuri katika mapambano yao.
“Tunapaswa kupeleka mchezo wa ndondi katika hatua kubwa, hii zawadi ya gari itaenda kwa mshindi ambaye atamchakaza mwenzake.
“Hili litakuwa pambano la kwanza la ndani kwa bondia kupata mafao makubwa, maana atapata gari na mkataba aliosaini,” amesema Semunyu.
Na AMINA KASHEBA