BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Twaha Kiduku, amesaini mkataba wa kupanda ulingoni kuzichapa dhidi ya Alex Kabangu kutoka DR Congo katika pambano litakalopigwa Machi 26, mwaka huu mkoani Morogoro.
Kiduku atapanda ulingoni katika pambano hilo la kimataifa dhidi ya Kabangu baada ya kumchakaza bondia, Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’ Agosti mwaka jana lililopigwa katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam
Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo Kiduku, amesema sapoti anayopewa na watanzania inazidi kumpa uwezo wa kufanya vizuri katika kila pambano huku akiahidi kuiandika historia kwa mara nyingine kwa kumchakaza Kabangu.
“Ni kweli nimesaini kucheza pambano hilo ambalo litakuwa la mkanda wa ubingwa, naamini mkanda utabakia kwa sababu lazima nifanye maandalizi ya kutosha chini ya kocha wangu Pawa Ilanda na nguvu kubwa ninayopewa na mashabiki zangu kwanza wa Morogoro na watanzania wote kwa ujumla ambao hawajawahi kuniacha tangu siku ya kwanza.
“Kila kitu tayari kimeshapangwa na promota juu ya siku ya pambano lakini maombi yangu ni kuweza kuwezasha pambano kufanyika mjini ili watu wengi waweze kuhudhuria taofauti na Magadu kwa sababu ni mbali na mjini, ” amesema
Muandaaji wa pambano hilo kutoka kampuni ya Peaktime, Meja Selemani Semunyu, ameeleza kuwa pambano hilo la kimataifa litasindikizwa na mabondia nyota wa Morogoro wakiwemo Joseph Mchapeni dhidi ya Ally Mwerangi, Juma Misari dhidi ya Kareem Mandonga.
Na AMINA KASHEBA