Na AMINA KASHEBA
BONDIA wa ngumi za kulipwa, Twaha Kiduku, anatarajia kupanda ulingoni kuzichapa na Tshibangu Kayembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Pambano hilo lisilo la ubingwa la raundi 10 uzito wa kati, linatarajiwa kufanyika Machi 19, mwaka huu katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.
Promota wa pambano kutoka kampuni ya Mopao, ambao ndio waandaaji, Ernest Mopao, amesema maandalizi ya pambano yanaendelea vizuri.
“Maandalizi yamekamilika kwa asilimia 95, mabondia watapima uzito wiki ijayo baada ya Kayembe kuwasili nchini, tunatarajia litakuwa pambano litakalovuta maelfu ya mashabiki wa ngumi nchini,” Ernest Mopao.
Mopao amesema licha ya pambano hilo, kutakuwa na pambano lingine la ubingwa wa WBF kati ya Yonas Segu ‘Black Mamba’ na Mmalawi Hannock Phiri.
Amesema pambano hilo lenye uzito wa Light litakuwa la raundi 12.
Akizungumzia maandalizi ya pambano lake, Kiduku amesema anaendelea kujifua vikali ili ashinde katika raundi za awali.
“Bondia nitakayecheza naye ana rekodi nzuri, hivyo ni lazima nifanye mazoezi makali yatakayofanikisha ushindi,” Kiduku.
Mwanamasumbwi huyo amewaomba wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kumuongezea morali ya ushindi.