BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Selemani Kidunda, ameahidi kuibuka na ushindi dhidi ya Bondia,Tshimanga Katompa katika pambano la Ubingwa wa WBF, litakalofanyika Desemba 26 mwaka huu Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam, Kidunda amesema anataka kuonesha ulimwengu na watanzania kuwa hakuna bondia anayeshinda ndani ya ardhi ya Tanzania.
Kidunda ameeleza kuwa watanzania wategemee ushindi upo kwa kiwango kikubwa.
“Nimejiandaa vizuri na bado naendelea na mazoezi kuelekea katika pambano hilo ushindi upo kikubwa kusubiri siku ya pambano ifike.
“Nia ya ushindi ipo nitampiga Kamtopa kwa namna yoyote, kwa staili yoyote hatatoka kikubwa ni sapoti kutoka kwa watanzania,” alisema.
Muandaaji wa pambano hilo Mkurugenzi wa kampuni ya Peaktime Media, Kapteni Selemani Semunyu, amesema pambano kati ya Kidunda na Katompa ni pambano la ubingwa wa WBF, uzani wa kilo 76 la raundi 10.
Muandaji huyo amesema pambano hilo litakuwa la kulipa kisasi baada ya Katompa kumchapa Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’ na kuondoka na Ubingwa.
Semunyu amebainisha kuwa kabla ya pambano hilo kutakuwa na mapambano 10 ya utangulizi na sita yatakuwa ya kimataifa na kwamba yote yatafanyika katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.
“Nawashukuru sana wadhamini wote pia mnadhimu Mkuu wa Jeshi kwa kulisimamia pambano hili kuanzia mwanzo hadi mwisho na kusema ukweli bila yeye pambano hili lilikua na hatihati ya kufanyika,
“Ameahidi pia kama namba moja atashindwa kufika siku hiyo basi yeye anaweza kumuwakilisha na kuwa mgeni rasmi siku hiyo,” amesema
Mabondia wengine watakaopambana siku hiyo ni Ismai Galiatano dhidi ya Denis Mwale, Ibrahim Class atazichapa na Israel Kamwamba, George Bonalacha ataminyama na Hassan Milanzi, Paul Magesta atapigana na Oscar Richard na Viguli Shafii dhidi ya Ally Kilongola.
Wengine ni Hamis Kibodi atacheza na Iddy Jumanne, Grace Mwakamela atacheza na Ruth Chisale, Najma Isike watapimana nguvu na Leila Yazidu na Daniel Materu dhidi ya Haruna Swanga.
Na AMINA KASHEBA