KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kenani Kihongosi, amewaomba wananchi wa Jimbo la Ushetu, kutokubali kurubuniwa na wanasiasa wenye uchu wa madaraka wanaopita maeneo yao kuomba kura, badala yake wamchague Emmanuel Peter Cherehani wa CCM.
Kauli hiyo ameitoa wakati akimnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya (CCM), Cherehani, katika mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Mwabomba Kata ya Idahina.
Amesema CCM ndicho chama pekee kitakachowakomboa katika shida mbalimbali zinazowakabili kama maji, umeme, afya, elimu na miundombinu ya barabara.
Amesema CCM ndicho chama pekee chenye Ilani ya uchaguzi inayotekelezwa kwa sasa hivyo, ni muhimu wananchi wakamchagua mgombea anayetokana na Chama tawala ili waendelee kutatuliwa kero mbalimbali zilizo katika maeneo wanayoishi.
“Wapinzani hawana ilani, hawana ofisi, kwa ngazi za kijiji, kata, wilaya, mkoa na Taifa, sasa mkiwachagua mkipata shida, mnakwenda kuwapata wapi, msirubuniwe na watu wasiojulikana wenye uchu wa madaraka, chagueni mgombea wetu mwenye Ilani bora ambayo iko kazini,” amesema Kihongosi.
Amesema mgombea wa CCM ana uwezo wa kuwasiliana na viongozi mbalimbali wa kitaifa kama Rais na Waziri Mkuu na akasilizwa shida zake kwa wakati, lakini wa upinzani hawezi kupata nafasi hiyo, wasijaribu kumchagua kwa sababu hana mtu anayekwenda kufanya naye kazi bungeni.
“Sasa wanaomba ubunge na ilani ya uchaguzi inayotekelezwa hawana, msiwachague, wanataka kwenda kujinufaisha kwa maslahi yao binafsi, CCM imemleta Cherehani.
“Amepimwa na vikao vyote vya juu, ameonekana anafaa, mpeni kura Oktoba 9, mwaka huu, akaendelee kusimamia maendeleo ya Wana Ushetu,” amesema Kihongosi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, alisema jimbo hilo ni jipya, bado lina changamoto nyingi ambazo zinahitaji utatuzi wa haraka.
Amesema mwenye kufanya hayo ni Serikali ya Chama hicho kupitia mgombea wake Cherehani.
“Cherehani anafaa kuvaa viatu vya mtangulizi wake, marehemu Elias Kwandikwa, mchagueni akatekeleze shughuli za maendeleo kama ilivyokuwa awali, ni mwadilifu, mnyenyekevu na msikivu, ndiyo maana chama kimempa ridhaa ya kugombea jimbo hili,” amesema Mlolwa.
Nae Cherehani amesema kuwa, kama atapata ridhaa ya kuliongoza jimbo hilo, atahakikisha kero zinazowakabili wananchi, zinapatiwa ufumbuzi wa haraka ili waendelea na shughuli za uzalishaji mali pasipo vikwazo.
“Bado jimbo letu lina changamoto nyingi ambazo zinahitaji kutatuliwa, naombeni kura zenu ili niweze kuwatumikia, nawaahidi katika uongozi wangu, hakuna mwananchi wala mtumishi atakayenyanyaswa na mtu mwingine, nitawatumikia kwa weledi na uaminifu mkubwa,” alisema Cherehani.
Uchaguzi mdogo wa jimbo la Ushetu, unafanyika baada ya kufariki dunia kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Elias John Kwandikwa kufariki dunia, Agosti 03, mwaka huu.
Na SALVATORY NTANDU, USHETU