WAKATI Watanzania wakiendelea kujiandaa kwa ajili ya Sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu, Umoja wa Vijana (UVCCM) Taifa umezindua kampeni ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kujitokeza kuhesabiwa.
Katika kampeni hiyo zaidi ya vijana 3,000 kutoka Chama Cha Mapinduzi, wamejitokeza katika maandamano yaliyoanzia Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa hadi uwanja wa Mwembe Yanga, jijini Dar es Salaam, wakiwa na mabango mbalimbali yenye ujumbe wa kuhamasisha wananchi kujitokeza kuhesabiwa huku wakiwa wamevalia fulana za rangi mbalimbali zenye picha ya Rais Samia Suluhu Hassan,
Akizungumza baada ya kuzindua kampeni hiyo, Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Kenani Kihongosi, amesema kampeni hiyo itakuwa endelevu katika mikoa ya kanda ya ziwa, Kaskazini, kusini pamoja na Zanzibar.
Amesema umoja wa vijana una wajibu wa kuungana na serikali, kueleza wananchi juu ya umuhimu wa sensa ya watu na makazi katika kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Tumeona baadhi ya maeneo kuna changamoto, watu waliohesabiwa mwaka 2012 wengine hawakuhesabiwa, serikali inapotoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni kwa idadi ya watu walioandikishwa na kuhesabiwa, Siku ya leo tuna watu watatoa elimu na kutunga nyimbo kwa ajili ya kuhamasisha sensa
Kampeni hii tumeizindua Dar es Salaam, tutakwenda maeneo mengine na tutaifanya kampeni hii kwa ukubwa, lengo ni kuunga mkoa juhudi za serikali ya awamu ya sita na utekelezaji wa Ilani ili kuhakikisha serikali inatimiza wajibu wake wa kutambua idadi ya watu,’’ amesema.
Kenani amebainisha kuwa katika kampeni hiyo watajumuika na wataalamu mbalimbali kutoka serikalini, ambao wataeleza faida watakazopata wananchi juu ya umuhimu wa kuhesabiwa.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala, amesema, takwimu za watu waliopo sasa ni ya mwaka 2012, hivyo wameamua kuunga juhudi za serikali kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa sensa, huku akiwataka vijana kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi kuhesabiwa.
“Tukihesabiwa miundombnu itaboreshwa na hata tatizo la ajira kwa vijana litapata ukombozi, tunalalamika vijana hawana ajira lakini serikali ikitambua idadi yetu itajua namna gani itataua tatizo hili,’’alisema.
Naye Katibu wa CCM tawi la Tandale, Bundara Malima, amesema ni muhimu wananchi kujitokeza kuhesabiwa kwani takwimu za watanzan itairahisishia serikali kutenga bajeti kulingana a idadi ya watu waliopo.
Na BARAKA LOSHILAA