KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Taifa, Kenan Kihongosi, amewasili rasmi makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), jijini Dodoma huku akitaja masuala matano ya kutazamwa kwa kina.
Ameyataja masuala hayo kuwa ni matumizi ya mitandao ya kijamii, mikopo ya vijana, masuala ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na ajira kwa vijana.
Kadhalika ameonya tabia ya baadhi ya viongozi ndani ya umoja huo, kuanza michakato ya kupanga safu ya uchaguzi ndani ya UVCCM katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Kihongosi ameyasema hayo leo jijini Dodoma, alipozungumza na wapenzi, wanachama wa UVCCM waliojitokeza kumpokea katika ukumbi wa White House, Makao Makuu ya CCM.
“Nitoe onyo kwa wale wanaohusika kubeba wagombea waache mara moja, wasubiri muda ufike, ni jambo la aibu hasa kwa vijana kubeba mgombea,watu hao wamekosa heshima, tusubiri muda ufike Chama kitatangaza utaratibu.
“Kwa sasa tukibaini kuna mwanachama anafanya vitendo kama hicho,tutachukua hatua kwa sababu katika kanuni zetu zinajieleza wazi, pia kuna miongozo ya maadili na adhabu zipo dhidi ya wanaokiuka,” amesema.
MITANDAO YA KIJAMII
Kuhusu matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, Kihongosi amesema kumekuwepo na kasumba kwa baadhi ya vijana kutumia mitandao ya kijamii, kutukana viongozi na kuendesha mijadala isiyo na tija kwa taifa.
Amewataka vijana kutumia mitandao hiyo vizuri kwa kujipatia kipato na kupashana habari.
“Naamini vijana wengi wanatumia mitandao ya kijamii na katika mitandao, kuna mijadala isiyo na tija inaendelea ikiwemo ya kutukana viongozi wetu, natumia fursa hii kuwasihi vijana kutumia mitandao vizuri,” amesema.
MIKOPO YA VIJANA
Kuhusu ya mikopo ya vijana inayotolewa katika halmashauri, Kihongosi amebainisha bado hakuna mwamko kwa vijana kuchangamkia fursa hiyo ambapo aliwataka UVCCM kuanza kutoa elimu kwa vijana ili waamke.
Amesema serikali inatoa fedha hizo bila riba, lakini zimekuwa hazifiki kwa walengwa.
“Umri wa vijana ni miaka 35 kushuka chini, lakini kuna vikundi vya watu ambao wameungana na wana umri zaidi ya hapo wanachukua fedha hizo,” amesema.
WANAFUNZI WA VYUO VIKUU
Katibu Mkuu huyo amesema katika Bajeti Kuu ya Serikali mwaka ya 2021/2022, serikali imeongeza bajeti ya mikopo ya elimu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka sh. bilioni 400 hadi kufikia sh. bilioni 500.
Amesema lengo la kuongeza fedha hizo ni kuhakikisha wanafunzi wengi wanapata elimu ya chuo kikuu ili taifa liwe na wasomi wengi.
“Hayo ndio mafanikio ya serikali inayoongozwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonyesha dhamira ya kuwasaidia wanafunzi kufika mbali zaidi,” amesema.
AJIRA KWA VIJANA
Kihongosi amewahakikishia vijana kuwa serikali inatekeleza miradi makubwa ya kimkakati lengo ni kuhakikisha inatengeneza fursa nyingi ya ajira kwa vijana.
“Rais Samia aliongea na vijana huko Mwanza, aliongelea mambo mbalimbali ambayo yanagusa vijana kuhusu mifumo ya elimu, TEHAMA (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano), ajira na sera ya vijana katika kilimo na fursa mbalimbali ambazo vijana wameshindwa kuzichangamkia,” amesema.
Na Happiness Mtweve