KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kenani Kihongosi, amewaomba wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro Mkoani Arusha, kumchagua mgombea wa chama hicho Emmanuel Shangai kwa sababu chama hicho kinatekeleza ilani yake kwa ufasaha.
Uchaguzi huo mdogo wa jimbo la Ngorongoro, unatarajiwa kufanyika Desemba 11, mwaka huu, baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Willium Ole Nasha kufariki Dunia hivi karibuni.
Kihongosi alisema hayo, wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni uliojumisha wananchi wa kata ya Ngoile na Orbalibali katika viwanja vya Mnadani vilivyopo Kata ya Ngoile.
“Wananchi wa Orbalibali na Ngoile kuna wagombea wa vyama 11 wamejitokeza kugombea ubunge katika jimbo hili.
Naomba niwaambie kwamba Ilani inayotekelezwa kwa sasa na serikali ni CCM, hivyo naomba kura zote apewe Shangai ili aweze kutatua changamoto zinazowakabili,” alisema.
Kihongosi alisema kata hizo zinakabiliwa na changamoto za barabara, huduma za afya , elimu na maji na kwamba mwarobaini wa matatizo hayo ni Shangai kwa sababu ataziwasilisha bungeni kikamilifu ili zifanyiwe kazi kikamilifu.
“Chagueni mgombea mnayemjua ambaye na nyie anawajua na mgombea huyo siyo mwingine ni Shangai kwa sababu mnaishi naye hapa Ngorongoro lakini pia amekuwa Diwani na Mwenyekiti wa Halmashauri yenu ya wilaya ya Ngorongoro na amepigania maslahi yenu na ninyi ni mashahidi,”.
Alisema Rais Samia anawapenda wananchi wa Ngorongoro na ana imani kubwa na Shangai mpelekeni bungeni ili akawe sauti ya kuzisemea changamoto zenu zinazowakabili kwa sababu ni kijana hodari, shupavu ,mnyenyekevu na mpenda maendeleo ya wananchi wa jimbo la Ngorongoro.
Akiwaomba kura wananchi hao, Shangai alisema kata ya Ngoile inakabiliwa na changamoto kubwa ya barabara ambapo kwa miaka 15 haijawahi kutengenezwa na kwamba wakimchagua mbunge wao atahakikisha Tsh. milioni 240 zilizotengwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) zinakarabati barabara hiyo kabla ya mwaka wa fedha wa serikali 2021-2022 inakamilika.
“Ninajua katika kata hii ya Ngile mnakabiliwa na changamoto ya maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu pamoja na mifugo naomba niwahakikishie kwamba serikali imetenga kiasi cha Tsh. milioni 200 kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu cha maji na kuyasambaza katika kata hii na mimi mkinipa ridhaa ya kuwa mbunge wenu changamoto hii nitaimaliza”alisema .
Alisema endapo atapata ridhaa ya kuwa mbunge wao, atahakikisha anamaliza changamoto ya huduma za afya katika kata hiyo na kuahidi kujenga nyumba ya watumishi katika zahanati inayojengwa katika kata hiyo.
“Halmashauri imetenga kiasi cha sh. milioni 50 kwa ajili ya kupaua jengo la zahanati na mimi ninawaahidi kwamba nitajenga nyumba ya watumishi ili huduma za matibabu zipatikane usiku na mchana”.
Kuhusu chagamoto ya maji katika Kata ya Orbalibali aliahidi kuchimba kisima cha maji katika eneo la Lemata ambayo yatasaidia wananchi kupata maji ya mifugo na matumizi ya nyumbani.
Alisema kata hizo, pia zinakabiliwa na majengo chakavu katika Shule za Msingi na Sekondari pamoja na upungufu wa waalimu hivyo atahakikisha anashirikiana na serikali kukarabati miundombinu ya shule hizo pamoja na kuleta waalimu ili kuongeza ufaulu zaidi.
NA LILIAN JOEL, Ngorongoro



























