Na Happiness Mtweve, Mafinga
KATIKA kutekeleza agizo la Amiri Jeshi Mkuu na Rais Dk. John Pombe Magufuli ya kuyataka majeshi nchini kujitosheleza kwa uzalishaji na kuwa na chakula cha kutosha na ziada, Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa 841KJ, Mafinga, mkoani Iringa kimejipanga kuhakikisha kinaboresha ufugaji na kilimo ili kuweza kinajitosheleza kwa asilimia 100 na kuondokana utegemezi kutoka Serikali Kuu.
Pia kimejidhatiti kuboresha shughuli za ufugaji kwa kuongeza Ng’ombe 100 wa maziwa ili waweze kukamua lita 1,000 za maziwa kila siku ambapo kwa sasa wana Ng’ombe 29 wanaokamuliwa kati ya Ng’ombe 120 walionao.
Kaimu Kamanda wa Kikosi hicho, Luteni Kanali Issa Chalamila, amesema hatua hiyo ni katika kutekeleza azma ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Charles Mbuge ya kutaka vikosi vyote vihakikishe vinajitosheleza kwa chakula.
“Huu ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Jeshi la JKT, Meja Generali Charles Mbuge la kutaka tujitegemee katika kujilisha bila kuitegemea hata Senti moja kutoka serikali, agizo hilo linatokana na agizo la Amiri Jeshi Mkuu na Rais Dk. Magufuli alilolitoa hivi karibu.
“Rais aliagiza majeshi tujikite zaidi katika masuala ya uzalishaji kupitia Kilimo na Ufugaji ili yaweze kujitegemea katika masuala mbalimbali bila kutegemea Fedha kutoka Serikali Kuu,” amesema
Ameongeza kuwa, licha ya kwamba kikosi chao kilianzishwa mahususi kwa ajili ya ufugaji lakini hivi Sasa wanafanya na shughuli za kilimo ambapo wamelima ekari 500.
Pia amefanua kuwa miongoni mwa mikakati iliyowekwa na kambi hiyo ni kuanzisha kilimo cha zao Parachichi kuongeza eneo la kilimo kutoka ekari 200 hadi 500 na kuongeza uzalishaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo.
MIFUGO
Kuhusu mifugo amesema kwa sasa wana zaidi ya Ng’ombe 120 ambapo kati ya hao Ng’ombe 29 wanaokamuliwa kila siku na wanatoa lita 200 hadi 250 za maziwa.
“Lengo letu ni kuboresha shughuli za ufugaji ili waweze kuzalisha maziwa mengi watakayoweza kuwalisha wananchi wa Mafinga na nje ya mafinga ambapo wanatarajia kuongeza Ng’ombe 100 ambao watakuwa na uwezo wa kuzalisha lita 1000 za maziwa kila siku,” Luteni Kanali Issa Chalamila
Amebainisha kuwa kwa upande wa mbuzi kwa Sasa wanao mbuzi 192 na mpaka Juni mwaka huu watakuwa wamefikisha mbuzi 300.
Luteni Chalamila amesema kwasasa wana zaidi ya Ng’ombe wa kienyeji 280.
Naye Luteni Francis Breck ambaye ni Mtaalam wa Mifugo katika kambi hiyo amesema kituo kina Ng’ombe wa aina mbili ambao ni Asher na Fishen na wana ekari 22 za malisho ya Mifugo hiyo ambazo wanazitumia zaidi kipindi cha kiangazi.
Amesema ili kuwa na malisho ya uhakika wanatarajia kuongeza ekari 50 za malisho ya majani ya kupanda.
“Umahiri wa mafunzo yenye weredi yanayotolewa katika Kikosi hichi, vijana wanaopitia mafunzo katika kambi hii wanakuwa mabalozi wazuri wenye uzalendo, wachapa kazi pindi wanaporudi uraiani,” amesema Luteni Francis Breck