HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH), inatarajia kujenga kituo cha umahiri cha kutoa huduma za
utengamao kwa wagonjwa wa afya ya akili katika Kijiji cha Vikuruti kikichopo Kata ya Chamazi Manispaa ya Temeke.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi, katika maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani ambayo hufanyika kila mwaka, Oktoba 10. Alisema MNH ina eneo Vikuruti lenye ukubwa wa
ekari zaidi ya 160, hivyo kuna nafasi ya kutosha kujenga kituo hicho cha umahiri kwa ajili ya matibabu ikiwemo wananchi wa kawaida ambao watahitaji muda wa pekee wa kutulia na kufanya tafakari binafsi.
Alisema kituo hicho kitakuwa na majengo ya kisasa ya kupumzika, mandhari ya kuvutia, miradi mbalimbali ya kimkakati kwa ajili ya kusaidia wahitaji kama sehemu ya tiba kazi ikiwa ni maandalizi ya kumrudisha kwenye jamii mgonjwa husika.





























