Na REHEMA MOHAMED
MAHAKAMA ya Tanzania imeanzisha kituo jumuishi kitakachoshugulikia mashauri ya mirathi, ndoa na familia, Mkoa wa Dar es Salaam, ili kuwezesha upatikanaji wa haki kwa haraka na wakati.
Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Messeka Cheba, ameyasema hayo, mbele ya kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria na kuongeza kwamba, kituo hicho kilichojengwa Temeke, Dar es Salaam, kitajumuisha wadau na wadaawa wote muhimu wa kesi hizo.
Amesema katika utafiti walioufanya mwaka 2017/18, walibaini pamoja na mambo mengine, kulikuwa na mashauri zaidi ya 5,000 ya masuala ya mirathi, ndoa na familia, hivyo Mahakama ikaamua kuanzisha kituo hicho katika majengo yake sita iliyojenga kama vituo jumuishi.
Chaba, amesema kituo hicho kitakuwa kikisikiliza shauri kwa siku saba hadi kutolewa hukumu, tofauti na ilivyo sasa, ambapo shauri humalizika ndani ya mwezi mmoja.
“Tumeanzisha kituo hiki kutokana na utafiti tulioufanya, ambapo tulibaini kuwepo kwa mlundikano wa mashauri mengi ya mirathi na masuala ya familia. Mkoa wa Dar es Salaam umeonekana kuwa na changamoto kubwa katika mashauri haya,” Messeka Cheba
Ameongeza kuwa kituo hicho kitajumuisha wadau wote muhimu katika uendeshaji wa mashuri hayo wakiwemo wanasheria.
Chaba, amesema kituo hicho jumuishi kitachochea haki kwa haraka na wakati, kuondoa urasimu, kupunguza na ucheleweshaji wa mashauri kama hayo.
“Changamoto ya ucheleweshwaji wa mashauri haya huchangiwa na mambo mbalimbali, ikiwemo wasimamizi wa mirathi kutotekeleza majukumu yao. Ucheleweshwaji wa mashauri haya pia husababisha kero na changamoto kwa ukiukwaji wa haki za watoto,” Chaba
Amesema huduma zitaanza kutolewa mara baada ya utaratibu wa kisheria kukamika na kwamba mchakato wa kutengeneza kanuni na mwongozo wa utendaji kazi wa kituo hicho umeshakamilika.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Mwigulu Nchemba, pamoja na mambo mengine, ameiasa jamii na Watanzania kwa ujumla ili kujenga utaratibu wa kuweka kumbukumbu na kurasimisha vitu kisheria ili kupunguza migogoro.
Dk. Nchemba, amesema Watanzania wengi hufanya vitu kwa kuaminiana na udugu katika masuala mbalimbali, ikiwemo biashara, ardhi na mmoja kati yao akivunja uaminifu, wanaingia katika migogoro pasi kuwa na kumbukumbu.
“Kutokana na kasi ya uaminifu kupungua, ni vyema kujenga njia ya kuwatendea haki wanaostahili. Ubaya wa kutoweka kumbukumbu unaleta matatizo kwa watoto,” Dk. Nchemba
Mbunge wa Mwanga, Joseph Tadayo, amesema kuwepo kwa kitengo maalumu cha mahakama cha masuala ya familia ni kilio cha muda mrefu kwani ni miongoni mwa kero wanazokumbana nazo wananchi, hasa vijijini.