Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewataka Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kuangalia namna watakavyoweza kutoa huduma ya kivuko huku wakizingatia Uchumi wa wananchi wanaotumia kivuko cha MV Musoma kinachofanya safari zake kati ya Mwigobero (Musoma) na Kinesi (Wilaya ya Ryorya) mkoani Mara.
Bashungwa amesema hayo leo tarehe 10 Oktoba 2023 akiwa kwenye ziara yake ya ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na wizara hiyo pamoja na kutatua changamoto zinazowapata watumiaji wa kivuko hicho baada ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hasan kutoa fedha ya ukarabati wa kivuko hicho.
Akiwa katika kivuko hicho moja ya changamoto zilizoelezwa na watumiaji wa kivuko hicho mbali na tatizo la kukosa jengo la abiria, kero nyingine ni utozwaji wa fedha kwenye mizigo ya kawaida ambapo Bi. Elizabeth Innocent anayefanya biashara ya maziwa kutoka Kinesi na Musoma amesema hutozwa fedha kiasi cha shilingi 200 kwa madumu yenye maziwa na shilingi 100 kwa madumu tupu.
Bashungwa amewataka Watendaji wa TEMESA kuwa na huruma na kukaa na Mkuu wa wilaya na wadau ili kuona namna bora ya kusaidia kupunguza machungu ya tozo kwa watumiaji wa kivuko hicho.
“Mkuu wa Wilaya, kaa na wasismamizi wa kivuko hiki muangalie hali ya wananchi na muweke utarajibu ambao unalenga kumnyanyua mwananchi na sio kumdidimiza, na muwe mnaomba miongozo sio mnaamua kuweka utaratibu wenu huku mwananchi akilaumu serikali” amesisitiza Bashungwa.
Kuhusu jengo la abiria, Bashungwa amesema kuwa Mheshimiwa Rais ameshatoa fedha muda mrefu lakini bado ukamilishwaji wa jengo hilo umekuwa ukizorota kwani jengo hilo lilitakiwa liwe limekwishakamilika na wananchi hao wanapata huduma nzuri wakati wanasubiri kivuko.
Bashungwa ametoa siku kumi kawa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wafike eneo hilo na wawe wametoa jawabu la namna ya kukamilisha ujenzi wa jengo hilo kwa asilimia 100 ifikapo Disemba mwaka huu.
Kukamilika kwa jengo hilo ambalo utekelezaji wake umefikia asilimia 35 litakalokuwa na uwezo wa kuchukua abiria zaidi 220 waliokaa.