Na REHEMA MOHAMED
MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Ardhi, imemtaka Mchungaji wa Kanisa la City Christian Fellowship (CCF), lililopo Sinza Palestina, Dar es Salaam, kufikiria namna ya kulipa deni la sh. milioni 139, anazodaiwa na Prosper Rwenyendera kama ilivyowasilishwa mahakamani hapo.
Pamoja na hilo Mahakama hiyo imemtaka Rwenyendera kubadilisha maombi yake ya kutaka kumpeleka gerezani Mchungaji huyo kwa kushindwa kulipa deni hilo, badala yake awasilishe maombi ya kukamata mali.
Kesi hiyo jana ilisikilizwa mahakamani hapo mbele ya Naibu Msajili Safina Semfukwe, ambapo kwa mujibu wa Mchungaji huyo ameieleza Mahakama kwamba kwa sasa hana uwezo wa kulipa kiasi hicho cha fedha.
Alidai, alikutana na wakili wa mdai (Rwenyendera) na kumueleza mpango wake wa kulipa deni, kwamba amlipe jumla ya sh milioni 12 sawa na sh 200,000 kwa mwezi.
Amedai, kwa sasa hana chanzo cha fedha cha kumuwezesha kupata fedha za kulipa deni hilo sh. milioni 139, kwani kanisa alilokuwa akitegemea limetawanyika na anapata fedha anapotoa mada sehemu.
Akijibu hoja hizo Wakili wa Mdai (Rwenyendera), Evodius Rutabingwa, alidai ni kweli mdaiwa aliomba kupunguziwa deni kutoka sh. milioni 139 hadi sh. milioni 12.
Wakili Rutabingwa alidai kwa mazingira ya kesi hiyo, mteja wake alikataa ombi hilo na kuomba alipwe kiasi hicho kama ilivyoamriwa na Mahakama na akishindwa wanaomba amri ya kumpeleka gerezani.
Baada ya maelezo hayo, Naibu Msajili alishauri wakili wa mdai kubadili maombi ya kumpeleka mdeni gerezani, hata kama wana uwezo wa kumhudumia mdai gerezani na badala yake waweke ombi la kukamata mali kwanza.
Hata hivyo, baada ya msajili kusema hivyo, mchungaji alidai nyumba anayo lakini ya familia.
Msajili alisema hata kama nyumba ya familia inaweza kukamatwa kwa kuwa kesi hiyo inamhusu yeye kama mdaiwa wa kwanza na kuwa mkewe anajua kila kinachoendelea katika kesi hiyo.
Sambamba na hilo, Msajili alimshauri mchungaji kuangalia namna ya kulipa deni hilo kabla Mahakama haijakamata nyumba yake, kwani mdai pia ni mwanadamu anaweza kubadili uamuzi wake.
Katika kesi hiyo, Aprili mwaka 2016 Mahakama hiyo mbele ya Jaji John Mgeta, iliamuru kanisa hilo lililopo Sinza Palestina Dar es Salaam, liondolewe mara moja na mdai apewe eneo lake
Ilidaiwa kanisa hilo lilijengwa tangu mwaka 2004 ambapo mchungaji huyo anadaiwa kushindwa kulipa kodi. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 12, mwaka huu.