Na MUSSA YUSUPH, KILOSA
WAKATI mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), kipande cha Dar es Salaam- Morogoro, ukiwa umekamilika kwa zaidi ya asilimia 98, serikali imesema reli hiyo itakuwa na uwezo wa kumudu mahitaji ya nchi kwa zaidi ya miaka 100.
Imesema safari za majaribio ya treni hiyo yenye kutumia nishati ya umeme, zinatarajiwa kufanyika Julai, mwaka huu, baada ya kuwasili vichwa na mabehewa mwezi Juni, huku safari rasmi za Dar es Salaam- Morogoro, zikitarajiwa kuanza Agosti, mwaka huu.
Akizungumzia ujenzi huo juzi, mkoani Morogoro, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dk. Leonard Chamuriho, alisema reli ya SGR inayojengwa nchini, ina viwango vya kimataifa, vyenye kuifanya kuwa miongoni mwa reli chache bora barani Afrika na kuzipita baadhi ya nchi za Mataifa ya Ulaya.
“Teknolojia iliyotumika kujenga reli hii ndio imeifanya kuwa reli bora Afrika na kuzipita baadhi ya nchi za Ulaya, zenye reli ya SGR, kwa sababu teknolojia za ujenzi zimebadilika,” alieleza.
Alisema ujenzi wa kipande cha awamu ya kwanza cha Dar es Salaam-Morogoro, umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90, na kwa sasa yapo maeneo machache ujenzi wake unamalizika.
“Baadhi ya maeneo ambayo bado hayajamilika, mfano kwenye sehemu za kuunganisha madaraja ya reli na barabara na sehemu nyingine miundombinu ya umeme, vyote hivyo tutavikamilisha ndani ya muda mfupi ili mwezi wa saba tufanye majaribio na mwezi wa nane treni ianze kufanya kazi,” Dk. Chamuriho, alieleza.
Waziri huyo wa Ujenzi na Uchukuzi, alisema Watanzania watarajie gharama nafuu za usafiri kuliko nauli zinazotozwa kwenye usafiri wa mabasi na kusisitiza kuwa, reli hiyo ina uwezo wa kuhimili mahitaji ya nchi kwa miaka 100 ijayo.
Vilevile, alisema reli hiyo itajengewa uzio ili kuzuia muingiliano wa reli na shughuli za kibinaadamu.
UBORA WA RELI
Akizungumzia ubora wa reli hiyo, Dk. Chamuriho, alisema reli ya Tanzania ina viwango vya kimataifa, ikilinganishwa na zingine zilizojengwa kwenye baadhi ya nchi jirani.
Alisema treni ya SGR ya Tanzania ina uwezo wa kwenda mwendokasi wa 160 kwa saa.
Mbali na hilo, alisema ubora wa reli hiyo umeifanya kuwa na uwezo wa behewa moja kubeba lingine kwa juu, kisha kuhimili uzito wa tani 35, kwenye kila mzigo (axle).
KENYA
Kwa mujibu wa mtandao wa wikipedia, reli ya SGR ya Kenya ina uwezo wa kwenda mwendokasi wa 120, kwa saa.
Kadhalika, mtandao huo unaeleza kuwa reli hiyo haitumii nishati ya umeme na uwezo wake wa kuhimili uzito wa mizigo ni tani 25, kwa kila mizigo.
Kwa sasa reli hiyo inatumika kusafirisha abiria na mizigo kutoka Mombasa-Nairobi.
ETHIOPIA
Ethiopia ilikamilisha ujenzi wa reli ya SGR, mwaka 2018, inayoanzia mji mkuu wa nchi hiyo, Addis Ababa hadi Read Sea State (Djibouti).
Kwa mujibu wa mtandao wa wikipedia, reli hiyo inayotumia nishati ya umeme, mwendokasi wake ni kilometa 120, kwa saa huku uwezo wa kuhimili mizigo ni tani 25, kwa kila mzigo.
MKURUGENZI MKUU TRC
Akizungumzia hatua za ujenzi wa reli hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, alisema ujenzi wake unazingatia kanuni zote za ubora huku malighafi nyingi zinazotumika zinatoka nchini.
Alisema ubora wa malighafi zinazotumika kwenye ujenzi huo, kuanzia mataluma, nondo, mchanga, saruji na kokoto, vinapimwa kwenye maabara maalumu.
Alisema kwa sasa, kiwanda cha kuzalisha mataluma ya reli ya SGR cha Dodoma, kina uwezo wa kuzalisha matuluma 1,500, kwa siku huku kiwanda kingine kilichopo Kilosa, mkoani Morogoro, nacho kina uwezo wa kuzalisha mataluma zaidi ya 1,000, kwa siku.
“Kwenye mkataba tuna makubaliano kwamba, kiwanda cha kuzalisha mataluma cha Kilosa, kitabaki kuwa cha serikali. Na uzuri ni kwamba, kiwanda hicho kina uwezo wa kuhamishika na hata pale tutakapokuwa na ujenzi wa reli ya SGR kwenye maeneo mengine, tutakihamishia huko,” alieleza.
Kadogosa, alisema awali wakati ujenzi wa reli hiyo ukianza, idadi kubwa ya wafanyakazi walikuwa kutoka nje ya nchi, lakini sasa asilimia 80, ya wafanyakazi kwenye mradi huo ni Watanzania na wageni wakiwa asilimia 20.
STESHENI YA SGR MORO
Akieleza hatua zilizofikiwa za ujenzi wa stesheni hiyo, Kaimu Meneja Msaidizi wa Mradi Stesheni ya Morogoro, Simon Mbaga, alisema stesheni hiyo imekamilika kwa zaidi ya asilimia 98.
Alisema stesheni hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 185, watakaokuwa wamekaa kwenye viti na zaidi ya abiria 400, watahudumiwa kwa wakati moja.
Alisema stesheni hiyo ina eneo lenye mita za mraba 8,400, zitakazotumika kuhifadhi makontena na mizigo mingine.
Pia, itakuwa na vibanda vitano vya kutolea huduma mbalimbali, migahawa minne na eneo la kuegesha magari madogo 180, mabasi sita na malori matano.
VICHWA SOGEZA
Akiwa kwenye karakana kuu ya reli pamoja na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Kadogosa, alieleza kukamilika kwa ukarabati wa vichwa saba vya treni, maarufu kama sogeza, ambavyo vilinunuliwa na serikali ya awamu ya kwanza, mwaka 1970.
Alisema vichwa hivyo baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu za kusogeza mabehewa na kuunganisha treni, vilikufa na kusababisha TRC kutumia vichwa vikubwa ya treni kufanyakazi hiyo.
Alisema shirika hilo lilikuwa likitumia vichwa vikubwa vya treni kufanyakazi hiyo, ambavyo vilikuwa vikitumia kiasi kikubwa cha mafuta, badala ya kutumika kuvuta mabehewa ya abiria na mizigo kwenda mikoa mbalimbali nchini.
Kadogosa, alieleza kuwa baada ya serikali kutoa fedha ya kukarabati vichwa hivyo, kwa sasa vina uwezo wa kuvuta mabehewa 10, badala ya nane na vinatarajiwa kufanyakazi hiyo kwa zaidi ya miaka 24.
“Tumetumia dola 800,000, badala ya kutumia dola milioni 1.3.
Jumla tumetumia dola milioni 5.8, kukarabati vichwa hivi na kama tungenunua vipya, tungetumia dola milioni 10.1,” alieleza.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa TRC, alisema vichwa hivyo vitakuwa na uwezo wa kufanyakazi kwa asilimia 80.
Kadhalika, alibainisha kuwa mbali na kutumika kusogeza mabehewa na kuunganisha treni, pia vitatumika kusafirisha abiria kwenye safari za treni za Dar es Salaam.
Vilevile, vichwa hivyo vitatumika kuvuta mabehewa ya mizigo, hususani makontena kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda bandari kavu ya Ubungo ili kupunguza msongamano wa mizigo kwenye bandari hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRC, Profesa John Kondoro, alisema mradi huo upo kwenye hatua nzuri , bado kazi ndogo kwenye kipande cha awamu ya kwanza ili kukamilika.
Alisema kuna baadhi ya maeneo, hususan Dar es Salaam, imelazimika kupisha baadhi ya miundombinu ili mradi huo uendelee.
MWENYEKITI KAMATI YA BUNGE
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, alisema kamati hiyo imeridhishwa na ujenzi wa mradi wa treni ya SGR.
Kakoso, ambaye ni Mbunge wa Mpanda Vijijini (CCM), alisema yapo mambo ambayo wamekuwa wakiishauri serikali na tayari yamefanyiwa kazi, ikiwemo malipo ya fidia kwa wananchi walioguswa na mradi huo.
Kadhalika, alisema kwenye mradi huo, kulikuwa na idadi kubwa na wageni waliokuwa wanafanya kazi, lakini baada ya kuishauri serikali ni asilimia 80 ya Watanzania wanaofanya kwenye SGR.
Hata hivyo, Kakoso, aliiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kuzingatia kuwaajiri vijana wanaojitolea kufanya shughuli za kiufundi kwenye karakana za TRC.
“Kumekuwa na utaratibu hawa vijana, ambao wanafanyakazi za kujitolea kwenye karakana zenu hamuwaajiri, mnawaajiri wengine. Sasa nawaagiza mzingatie vijana hawa wanaojitolea,” alieleza.
Akitolea majibu agizo hilo, Waziri wa wizara hiyo, Mhandisi Chamuriho, alisema suala hilo linapaswa kufanyiwa kazi na TRC, hivyo aliliagiza shirika hilo kuweka vigezo vya ajira vyenye kuzingatia vigezo vitakavyowezesha vijana wanaojitolea kuajiriwa.
Naye, Mjumbe kamati hiyo, Aeshi Hilary, alisema mradi huo utaleta manufaa makubwa endapo wananchi watautumia.
Hilary, ambaye ni Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), alisema licha ya wananchi kuutumia miradi huo kibiashara, miundombinu yake inatakiwa kutunzwa kwa maslahi ya taifa na wananchi kwa ujumla.
Mjumbe mwingine wa kamati hiyo, Mbunge wa Viti Maalumi (Chadema), Sophia Mwakagenda, alisema serikali imesimamia vyema fedha za wananchi katika kutekeleza mradi huo.
Alisema endapo fedha za wananchi zikiendelea kutumika vizuri, wabunge hawatakuwa na shida katika kuunga mkono utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini.
Naye, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mhandisi Mwanaisha Ulenge, alisema ili mradi wowote wa ujenzi ukamilike kwa vigezo vinavyohitajika, lazima usimamizi mzuri wa kihandisi ufanyike.
“Mradi huu umesimamiwa vizuri, naamini vijana walioshiriki wamejifunza mengi kuhusu teknolojia iliyotumika,” Mhandisi Aisha, alieleza.
MAONI YA WANANCHI
Baadhi ya wananchi walitoa maoni kuhusu mradi huo, ambapo walisema uamuzi wa kujenga reli ya kisasa umezingatia mahitaji ya taifa kwa maendeleo ya uchumi wa wananchi wake.
Mkazi wa Mazimbu, mkoani Morogoro, Lucas Minja, alisema ili uchumi wa wananchi wa taifa lolote uweze kuimarika, uwepo wa miundombinu imara ya uchukuzi ni mojawapo ya kigezo muhimu.
“Reli tuliyonayo sasa ni ya zamani, imejengwa tangu enzi za mkoloni, haikidhi mahitaji ya dunia ya sasa. Serikali kujenga reli ya SGR ni matokeo mazuri ya kuangalia maendeleo ya uchumi wa sasa na ujao,” alisisitiza.
Naye, Mikidadi Msindi, mkazi wa Morogoro, ambaye ni mkulima wa mazao ya viungo, alisema reli hiyo ikianza kufanyakazi, itawasaidia wakulima kusafirisha mazao kwa gharama nafuu.
“Kwa sasa tunapata wakati mgumu kusafirisha mazao yetu kwenda Dar es Salaam. Wenye maroli wanatutoza gharama kubwa, ikilinganishwa na kile ambacho tunakwenda kukipata sokoni, tunaamini usafiri huu wa reli utakuwa nafuu kwetu,” alisema.
Reli ya kisasa ya SGR inatarajiwa kuongeza ufanisi kwenye sekta ya uchukuzi ndani ya nchi na mataifa jirani ya Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
SGR imekusudiwa kuchukua nafasi ya mfumo wa reli ya zamani, ambapo inatarajiwa kupunguza msongamano wa barabara, ikiwemo gharama za usafirishaji kwa asilimia 40.
Kila treni ya mizigo inatarajiwa kusafirisha hadi tani tani 10,000, sawa na mizigo inayobebwa na maroli 500.
Mradi huo unatekelezwa kwa awamu tano, ambapo awamu ya kwanza (Dar es Salaam-Morogoro), awamu ya pili (Morogoro – Makutopora), awamu ya tatu (Makutopora-Tabora), awamu ya nne (Tabora-Isaka) na awamu ya tano (Isaka-Mwanza).