LEO ndiyo safari ya mwisho ya Josiah Ekwabhi Mufungo, mhariri mkongwe, ambaye ameacha historia ya kipekee katika tasnia ya habari nchini.
Ni ya kipekee kwani maisha yake yote tangu ujana hadi kustaafu, aliitumikia kwa uadilifu mkubwa Shirika la Magazeti ya Chama (SMC) ambalo baadaye lilibadilika na kuwa Kampuni ya Uhuru Publichations Limited (UPL), kuanzia mwandishi wa habari mwanafunzi, mwandishi wa habari, mwandishi wa habari mwandamizi, msanifu mwanafunzi, msanifu mkuu, mhariri, naibu mhariri mtendaji na mhariri mtendaji wa UPL.
Unaweza kusema kama ni mchezaji wa mpira wa miguu, basi alicheza namba zote kuanzia golikipa, mlinzi ‘beki’, kiungo wa kati na mshambuliaji wa kutumainiwa na mwenye uwezo mkubwa wa kubadili mchezo na kupata matokeo.
Si wengi wanaobahatika kutumikia taasisi kama hizi zetu za habari kwa mafanikio makubwa kama ilivyokuwa wa Chifu Mufungo, licha ya mitikisiko na mabadiliko makubwa ambayo vyombo vya habari nchini vilipitia kwa nyakati tofauti.
Ni Chifu Mufungo, ndiye aliyeshuhudia na wakati mwingine kuhusika moja kwa moja katika hatua mbalimbali za mabadiliko, ambayo UPL ilipitia kuanzia ikiwa ni Shirika la Magazeti ya Chama (SMC), lililokuwa likiendesha magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani.
Katika hili, napenda nirejee kipindi cha miaka 1990, ambapo vyombo vingi vya habari hususani magazeti yalianzishwa yakiwemo ya Nipashe na Majira, ambayo kwa kiwango kikubwa yalilidhoofisha Uhuru kwa kuchukua baadhi ya wahariri, waandishi waandamizi na wapiga picha.
Ulikuwa ni mtikisiko mkubwa kwani ‘dau’ lililotangazwa kwa wanataaluma hao lilikuwa kubwa, ikilinganishwa na mishahara na marupurupu ya Uhuru na Mzalendo kwa wakati huo kwa waandishi wake.
Ni wahariri na waandishi wengi nguli waliondoka Uhuru na Mzalendo kwenda ama kuanzisha au kusimamia magazeti hayo na kutoa ushindani mkubwa kwa soko la mauzo ya nakala za magazeti nchini.
Mufungo wakati huo akiwa ni msanifu mkuu na baadaye naibu mhariri mtendaji, hakuyumba, alikwenda na ‘jahazi’ la Uhuru likiwa na safu ndogo ya wahariri na waandishi wenye uzoefu, kuhimili ushindani wa soko la habari kwa wakati huo.
Kwa kweli ulikuwa mtikisiko wa aina yake, lakini naweza kusema ulifungua fursa kwa waandishi wengi, hasa vijana kupata ajira, kuongeza ushindani na hivyo kupanua wigo wa uhuru wa habari nchini.
Katika hilo, nakiri Chifu Mufungo alifanikiwa kuvuka salama na magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani kutopoteza ubora wala dira yake.
Kwa ufupi, magazeti hayo yalivuka kiunzi hicho salama chini ya uongozi mahiri wa Chifu Mufungo na kuendelea kujijenga na kujiimarisha hadi sasa ambapo gazeti la Uhuru lina zaidi ya miaka 60, tangu kuanzishwa kwake, likijivunia ukongwe, na historia ya kipekee katika tasnia ya habari nchini.
Kwa nilivyomfahamu Chifu Mufungo, naweza kusema alifanikiwa kuivusha UPL katika dhoruba zote hizo, kutokana na historia yake, ambayo imejikita katika utendaji makini, uadilifu, nidhamu na uzalendo usiotiliwa shaka.
Kwa kumbukumbu na maelezo ya Mhariri wa Habari mstaafu Joe Nakajumo, Chifu Mufungo alijiunga na Uhuru, wakati huo yakiwa ni magazeti ya Chama cha Tanganyika African National Union (TANU), mwaka 1973, akitokea Idara ya Ushirika katika Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Ushirika.
Kwa mujibu wa Nakajumo, Mufungo aliajiriwa siku moja na wenzake wakiwemo Hamis Daudi Mkwinda na Kohereth Magessa. Mhariri Mtendaji aliyewaajiri akina Mufungo na wenzake alikuwa Komredi Balozi Ferdinand Ruhinda.
NIDHAMU NA UTENDAJI
Wakati najiunga na Uhuru wakati huo (SMC), mwaka 1993, nikiwa mwandshi wa habari mwanafunzi, baada ya kumaliza kidato cha sita, Mufungo ndiye alikuwa msanifu mkuu wa magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani.
Chifu Mufungo aliipenda kazi yake kwani hakuwahi kukosa kikao cha ‘postmortem’ (mapitio ya magazeti kila asubuhi) pasipo na sababu za msingi, kwa kuwa ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho.
Anapoendesha kikao hicho, tambua kwamba ameshasoma habari na makala zote katika gazeti la Uhuru, pia ameshapitia baadhi ya magazeti mengine nje, hadi kupitia matangazo na penye kasoro atasema.
Kwa hiyo, hapo si wahariri, waandishi au wasanifu wa gazeti waliokuwa na ‘kibarua’ cha kujibu maswali yake, bali hata maofisa matangazo na usambazaji nao walikuwa sehemu ya ‘kiti moto’ hicho.
Alikuwa ni mhariri aliyekuwa akifika kazini mapema bila kujali jana yake alikuwa wa mwisho kutoka na muda huo, yeye na Chifu Joe Nakajumo, waliutumia kusoma magazeti mpaka ya nje kwa ajili ya kujiandaa na kikao cha ‘postmortem’.
Baada ya ‘postmortem’ aliingia kikao kingine cha bodi ya wahariri ambacho mbali na kujadili habari na makala zinazoandaliwa kwa siku husika, pia walikuwa wakizunguzia masuala ya uendeshaji hususani ndani ya idara ya habari.
Anapotoka katika kikao hicho muda wote atakuwa kwenye dawati la usanifu kuandika ama maoni au kupitia makala na kuandaa kurasa kwa habari za siku hiyo.
Pamoja na kwamba alikuwa na wasaidizi makini kama Chifu Godfrey Mhando (marehemu), Chifu Stephen Mganga (marehemu) na Chifu Hamis Mkwinda, daima alikuwa bega kwa bega nao, na wakati mwingine hata akiangalia vichwa vya habari vilivyosanifiwa na wasanifu wenzake na kushauri vinginevyo.
HAKUPENDA UZEMBE
Moja ya jambo ambalo hakupenda kuona likijitokeza ni uzembe na uvivu, kwa kuwa yeye mwenywe alionyesha kwa mfano kwa kufanya kazi hata za ziada na wakati mwingine kulazimika kufanya kazi za mhariri mwenzie pale anapoona kuna upungufu.
Chifu Mufungo hakupenda kuona gazeti linachelewa kufika kiwandani kwa ajili ya kuchapwa, na wakati mwingine alikuwa yuko radhi kuacha habari na kusema hiyo “haiwezi kutuchelewesha iandikeni kesho kwa ‘angle’ nyingine”.
Msingi wa kuwahisha gazeti mtamboni ilikuwa ni pamoja na kuhakikisha matangazo yaliyochapwa hayaathiriwi na gazeti kuchelewa, kwa kuwa moja ya vyanzo vya mapato katika magazeti ni matangazo.
Pia, Mufungo hakupenda waandishi ‘masilahi’ na alikuwa akikubaini una pendapenda vijibahasha basi wewe huna nafasi kwake. Kwa ufupi hakupenda habari yoyote ipindishwe au ipotoshwe kwa sababu zozote zile, ikiwemo ya ‘mshiko’.
Hivyo chini Mufungo, wahariri wenzake na waandishi wa habari wa Uhuru na Mzalendo, walikuwa ‘wamenyooka’ kwa msemo wa vijana wa siku hizi, kwani alikuwa mkali katika hilo.
MWALIMU
Moja ya sifa kuu ya Chifu Mufungo ilikuwa kupenda kufundisha wenzake, kuanzia wasanifu hadi waandishi, kwake haikuwa tatizo kuja mezani kwako na kufuatilia unachoandika, hata kabla hakijamfikia mhariri wa habari, hasa unapoandika habari kuu yaani ‘lead story’.
Wakati mwingine utamsikia akimweleza Mhariri wa Habari Nakajumo. ‘Joe hiyo nimeshaichukua’, hapo ujue anataka kuipitia kwa umakini zaidi na kuiwaisha gazetini.
Tukio ninalolikumbuka sana ni kipindi ambacho tunaelekea katika uchaguzi mkuu wa 2015, wakati huo licha ya kwamba alikuwa ameshastaafu tulimwita atupe semina ya namna ya kuripoti mikutano ya kampeni, alikuja na kutunoa vilivyo huku akitutakia kila la kheri.
Aidha, tukio lingine ni wakati wa kampeni pale nilipompigia simu kumuomba ushauri, baada kupokea habari kuu iliyokuwa na ‘kauli nzito’ za mmoja wa viongozi, Chifu Mufungo hakusita kunishauri na kuniongoza na hatimaye tukavuka salama.
Nakumbuka pia niliwahi kupitia changamoto ya tishio la mgomo wa wafanyakazi UPL, nikiwa kaimu mhariri mtendaji wa UPL, hilo nalo alinishauri na kunivusha salama ‘Asante Chifu Mufungo’. Nakumbuka; kwanza alinipa pole kwa changamoto hiyo na kuniambia kwa Kiingereza akichanganya na Kiswahili;
“Tumia any administrative measure, kuhakikisha gazeti linatoka, vinginevyo sina msaada zaidi,” muda huo ilikuwa ni saa 9.00 jioni, kukiwa hakuna habari yoyote iliyoandikwa na kuhaririwa.
ALIFUNDISHA NA KUAMINI VIJANA
Sifa nyingine kuu aliyokuwa nayo Chifu Mufungo ni kuamini vijana, pale anapokupima na kujiridhisha kwamba unaweza.
Katika vyumba vya habari uandishi wa Maoni ya Mhariri kutokana na unyeti wake na kwa kuwa yanabeba msimamo wa gazeti, mara nyingi huandikwa na wahariri au waandishi waandamizi.
Lakini kwa Chifu Mufungo ‘mwiko’ huo haukuwepo, kwani alipenda kumteua mwandishi mwandamizi mmoja na kumpa wazo la kuandikia maoni na upomaliza atayapitia na kukuambia uyasome kama si siku hiyo basi kesho yake.
Pia hakusita kumpendekeza mwandishi mwandamizi kijana, kushika dawati kama ilivyokuwa kwa waandishi vijana wakati huo, Godfrey Lutego kuwa mhariri wa michezo na baadaye Rashid Zahor, ambaye kwa sasa ni marehemu.
Jacqueline Liana naye ni miongoni mwa waandishi waandamizi waliofanya kazi chini ya Chifu Mufungo, akiwa ndiye mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Naibu Mhariri Mtendaji wa UPL, kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya, na sasa ni mtumishi wa CCM.
Hivyo, wakati leo tukiupumzisha mwili wa Chifu Mufungo, kwenye nyumba yale ya milele, itoshe kusema ameitendea haki taaluma ya habari nchini na mchango wake daima hautasahaulika.
BURIANI CHIFU MUFUNGO.
NA RAMADHANI MKOMA