Na LILIAN JOEL, Arusha
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile ametangaza kwamba kuanzia Juni 30, mwaka huu, laini zote za simu za kiganjani ambazo hazijasajiliwa kwa kutumia kitambulisho CHa Taifa zitaondolewa sokoni.
Pia, ametoa mwezi mmoja kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuanza kutoa leseni za usajili wa ‘blogs’ na luninga za mtandaoni na kupunguza gharama za usajili huo ili vijana wengi zaidi wajiajiri.
Pia, waziri huyo alitoa miezi mitatu kwa kampuni za simu nchini kurekebisha huduma za mawasiliano kwa wateja wao tofauti na sasa ambapo wateja wanapiga simu zinakoroma lakini wanakatwa fedha bila kupewa huduma.
Maagizo hayo aliyatoa jana akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu mkoani Arusha kama sehemu ya kuadhimisha siku100 za kuanzishwa kwa wizara hiyo ambayo kilele chake ni Machi 30, mwaka huu.
“Kuanzia sasa kila mwananchi ambaye hajasajili laini yake kwa kutumia kitambulisho cha Taifa (Kitambulisho cha NIDA) ahakikishe anasajili laini yake kabla ya Juni 30, mwaka huu, kwa sababu tutazima laini zote za simu ambazo hazijasajiliwa,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Ndugulile, serikali imeshatoa muda wa kutosha kusajili laini kupitia namba za NIDA, lakini bado kuna wananchi ambao hawataki kuchukua vitambulisho vyao au namba kwa ajili ya kusajili laini za simu.
“Ni kosa kisheria mtu kutumia kitambulisho chake kumsajilia mtoto wake laini ya simu au ndugu na kuanzia sasa wote waliofanya hivyo wabadilishe usajili huo mara moja na kufanya uhakiki kujua kama kitambulisho kimetumika kimakosa kusajili laini kupitia mfumo unaokiuka sheria unaofanywa na mawakala wanaosajili laini za simu,” alisema.
Kuhusu usajili wa blogs na luninga za mtandaoni, Dk. Ndugulile aliiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ikamilishe mara moja mifumo yake na ianze kutoa leseni za usajili ndani ya mwezi mmoja, badala ya Juni mosi, mwaka huu.
“Sikubaliani na ajenda yenu ya kutoa leseni Juni. Ni mbali sana nendeni mkajipange kwa kuweka mifumo yenu vizuri na baada ya mwezi mmoja leseni zianze kutolewa na kupunguza gharama za usajili,” alisisitiza.
Alisema vijana wengi wana nia ya kujiajiri kupitia mfumo huo, lakini wanakwamishwa na gharama kubwa za usajili wakati lengo la serikali ni kuona wengi wao wanajiajiri ili kujikwamua kuiuchumi.
“Natambua vijana wengi wanajitahidi kujiajiri kupitia luninga za mtandaoni na ‘blogs’ halafu TCRA mnaweka gharama kubwa. Rekebisheni gharama hizo mara. Rai yangu kwao wazingatie maudhui kulingana na sheria za nchi na siyo kujisajili ili kutumia mitandao hiyo kinyume cha sheria,” alisema.
Katika hatua nyingine, Dk. Ndugulile alituma salamu kwa mafundi wa simu za kiganjani na kuwataka kuacha mara moja tabia za kubadilisha ‘IMEI’ za simu zinazoibwa na kuonya watakaobainika kucheza mchezo huo mchafu watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Mafundi simu acheni mchezo mchafu zingatieni sheria nchi wakati wa kutekeleza majukumu yenu ya kila siku kwa sababu serikali ina uwezo wa kuzima simu zote zinazobadilishwa ‘IMEI’ na zisitumike hapa nchini,” alisema.
Awali, Meneja wa TCRA, Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Imelda Salum alisema ofisi yake kwa kipindi cha Juni, mwaka jana hadi Juni, mwaka huu imepanga kukusanya zaidi ya sh. bilioni 1.27 na mpaka sasa wamekusanya zaidi ya sh. milioni 810.
Mhandisi Imelda alisema TCRA inaendelea kutoa mafunzo kwa watumiaji wa simu na kwamba mafundi simu 332 katika Kanda ya Kaskazini wameshapatiwa elimu.