WASICHANA wa kazi za ndani maarufu kama ‘House Girl’ ni moja ya makundi muhimu katika jamii kutokana na majukumu makubwa wanayoyafanya.
Wamekuwa msaada mkubwa katika kutunza nyumba na kulea familia za waajiri wao.
Hata hivyo, wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi katika jamii inayowazunguka, baadhi yao hupata mikasa tofauti kutokana na kile kinachodaiwa kuwa manyanyaso kutoka kwa baadhi ya waajiri wasiojali umuhimu wao.
Umasikini na kushindwa kuendelea na masomo, kumetajwa ni mojawapo ya vyanzo vya wasichana hao kwenda katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma na Arusha kwa lengo la kufanya kazi hizo za ndani ili wapate vipato vya kuhudumia familia zao.
“Nimeteseka, nilitolewa nyumbani kwetu nikaambiwa nakuja mjini kusoma ‘tuition’, lakini mambo yakawa tofauti.
“Nilipelekwa kufanya kazi za ndani, nilipitia mateso mengi ikiwa ni pamoja na kutolipwa mshahara na kulazimishwa kushiriki ngono.”
Hivi ndivyo anavyosimulia Latifa Salumu, binti wa miaka 28 aliyepitia mikasa ya kunyanyaswa kijinsia, kufanyiwa ukatili wa kingono wakati akiwa na miaka 17 akifanya kazi kwa mwajiri wake wa kiume.
Latifa anasema mazingira ya kufanya kazi za ndani huwa shubiri unapokutana na mwajiri ambaye hana utu, upendo na hofu ya Mwenyezi Mungu katika kumjali binti wa kazi, baadhi yao huwaona hawana thamani kama walivyo watoto wao.
AFUNGUKA ALIVYOKABILIWA NA UKATILI WA KINGONO
Latifa, anasema baada ya kuajiriwa katika nyumba hiyo akiwa na miaka 17, mama mwenye nyumba, alikuwa anamwachia kufanya majukumu yote ya kutunza familia kwani hakuwa na muda wa kukaa nyumbani na familia yake.
“Mama ambaye ni mwajiri wangu, alikuwa ‘bize’ sana, akitoka nyumbani saa 11 alfajiri, anarudi usiku ilinilazimu mimi ndiye niwe mlezi wa mtoto wake mdogo,” anasema.
Mwanadada huyo anaeleza kuwa, alianza kukabiliwa na vishawishi vya mume wa mwajiri wake, alitafuta mwanya wa kuzungumza na mama huyo, lakini alikuwa hampi nafasi kutokana na kila alipomuomba kuzungumza naye, alijibiwa hana nafasi.
Anasema kitendo cha kutolipwa mshahara kwa kipindi cha miezi minane, kilimfanya aingie katika vishawishi na mitego ya baba mwenye nyumba ambaye alimfanyia vitendo vya ukatili wa kingono.
Wakati mama mwenye nyumba alipokuwa anaondoka nyumbani alfajiri, Latifa anasema alikuwa anamwambia akamchukue mtoto chumbani kwake ambako analala na mumewe.
Latifa anaeleza kwamba, alikuwa analazimika kila siku alfajiri kwenda kumgongea mume wa mama huyo ili kumchukua mtoto aanze kumuhudumia.
Kitendo cha kutekeleza maagizo ya mwajiri wake cha kumfuata mtoto kila siku chumbani, kiliibua changamoto na kutoa mwanya kwa mume wa mama huyo kuanza kumrubuni, hatimaye alifanyiwa ukatili wa kingono.
Latifa anasema baada ya kufanyiwa kitendo cha ukatili wa kingono, mama mwenye nyumba, aligundua ukatili aliofanyiwa na mumewe, hivyo alimfukuza katika nyumba hiyo bila kulipwa chochote.
“Niliondoka katika nyumba ile bila kulipwa fedha yoyote, kwanza nilikuwa nafanyakazi bila mkataba, maisha yangu yalikuwa magumu,” anasema Latifa.
Hata hivyo, Latifa anasema baada ya kuondoka katika familia hiyo, alipata kazi ya kufanya miamala ya simu, kazi ambayo hakudumu muda mrefu kwani hakuwa akilipwa ujira kwa wakati.
KUHUSU KIKUNDI CHA SAUTI YA JAMII
Latifa anasema kuwa, mwaka 2020 alibahatika kuhudhururia semina iliyohusu namna wasichana wa kazi za ndani kutambua haki zao, iliyoandaliwa na Taasisi ya Sauti ya Jamii iliyopo Kipunguni, Dar es Salaam.
Kupitia semina hiyo, Latifa alijifunza mambo mbalimbali zikiwemo haki za wasichana wa kazi za ndani kujua wajibu na haki zao za msingi.
ALIVYOANZA HARAKATI
Kupitia semina hiyo, Latifa anasema alipopata elimu na kujitambua thamani yake, aliamua kuanza kutafuta wasichana wa kazi za ndani kwa kupita nyumba moja hadi nyingine kuomba kuzungumza nao ili awape elimu.
Agosti mwaka huu, alianza harakati hizo maeneo ya Chanika, Dar es Salaam kupitia wajumbe wa nyumba 10 kutambua nyumba zenye wasichana walioajiriwa kufanya kazi za ndani, alianza na wasichna 20.
Anasema amekuwa akiwafundisha wasichana hao wa kazi za ndani kufahamu haki zao, kuhakikisha wanajua haki zao zikiwemo kuwa na mikataba ya ajira kutoka kwa waajiri wao.
MAFANIKIO YAKE
Latifa anasema tangu aanze kutoa elimu hiyo, amefanikiwa kutoa elimu hiyo kwa wasichana 40 na waajiri 30, anashukuru mwitikio umekuwa mkubwa na kuanzisha kikundi ambacho wanatoa elimu sehemu mbalimbali.
Kupitia mafunzo hayo, amefanikiwa kuwaeleza wanaowaajiri wasichana wa kazi za ndani, kutambua umuhimu wa mwanamke kukaa na kuzungumza wasichana hao, badala ya kuwatenga kwani hufanya hivyo kutasaidia kutatua changamoto mbalimbali.
Aidha, anasema katika mafundisho anayoyatoa, amekutana na wasichana 30 wanapitia changamoto mbalimbali kama ubaguzi, unyanyasaji na kutolipwa mishahara yao kwa wakati.
CHANGAMOTO
Latifa anasema changamoto anayokutana nayo ni baadhi ya waajiri wasivyokuwa na utu, kujenga chuki dhidi yake kutokana na elimu anayotoa kwa wasichana hao.
Changamoto zingine ni baadhi ya mabinti wanaopata elimu nyumbani kwake, kutokurudi kwa waajiri wao kutokana na waajiri kuwazuia kufanya hivyo.
MATARAJIO YAKE
Latifa anatamani kuwafikia wasichana wengi katika mikoa mbalimbali nchini ili watambue haki zao za msingi na namna bora ya kukabiliana na rushwa ya ngono na ukatili.
Anaomba ushirikiano kutoka kwa serikali na taasisi mbalimbali, zimwezeshe kuwafikia wasichana wengi zaidi wanaofanyiwa vitendo vya ukatili na waajiri wao.
WITO WAKE
Latifa anatoa ushauri kwa wasichana wa kazi za ndani kutokukubali kushawishiwa kufanyiwa ukatili wa kingono, badala yake, wanapoona mazingira yasiyofaa, watoe taarifa kwa mamlaka husika.
HISTORIA YAKE
Latifa ni binti mwenye umri wa miaka miaka 28 mzaliwa Shinyanga, alilelewa na mzazi mmoja kutokana na mama yake mzazi kupoteza maisha, akiachwa akiwa na umri wa mwaka mmoja.
Kutokana na mama yake mzazi kufariki dunia, baba yake alihamisha makazi kutoka Shinyanga kwenda Dar es Salaam, alianza elimu ya msingi mwaka 2000 katika Shule ya Msingi Kisanga, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.
Mwaka 2007 alianza elimu ya Sekondari katika Shule ya Mwanalumango, hukohuko Kisarawe na kuhitimu kidato cha nne mwaka 2010, baadaye alianza kufanya kazi za ndani.
Na IRENE MWASOMOLA