UUGUZI na ukunga ni muhimu katika kupunguza maumivu kwa wagonjwa, kuboresha huduma ya mama na mtoto na makundi mengine ndani ya jamii.
Kutokana na umuhimu huo Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto Dk.Dorothy Gwajima akizindua Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC), anasema baraza hilo lina wajibu wa kuhakikisha linalinda, kuimarisha na kuhifadhi afya ya jamii, usalama na ustawi, kupitia usimamizi na udhibiti wa shughuli za mafunzo ya uuguzi na ukunga.
“Wahitimu wamekuwa wengi na hawana stadi za kutosha, kumekuwa na utitiri wa vyuo na havina vigezo vya kutosha katika maeneo ambayo hayakidhi vigezo, vifaa kama serikali tutashughulika navyo,wale wanaosoma vyuo ambavyo havijasajiliwa wanajifurahisha maana hawatasajiliwa,”anasema.
Dk.Gwajima anasema, takribani asilimia 60 ya watoa huduma za afya nchini ni wauguzi na wakunga, ikilinganishwa na kada zingine.
“Tasnia hii inafanya kazi ya wataalamu wengine pale wapokuwa hawapo, unakuta wauguzi wanawapa wagonjwa dawa, wanakaa na watoto na kwa uzoefu wake unamhudumia mgonjwa, hivyo tunakila sababu ya kuwasaidia,’’anasema.
Dk.Gwajima anabainisha kuwa, ili kuboresha huduma inayotolewa na wakunga na wauguzi, ni muhimu TNMC kuandaa miongozo ya kutolea huduma na zipatikane mahala pa kazi.
“Hakikisheni miongozo hii inapatikana katika maeneo ya kutolea huduma na iwe rahisi mtu kuipata mitandaoni.
Kwa upande wa serikali, tutakwenda kuhakikisha tunaimarisha uwepo wa wauguzi katika vyombo vya maamuzi, kazi hii ni kubwa ya kusimamia na kutetea maslahi ya wauguzi kupitia sheria,”anaseama.
MAGEUZI KWA WAUGUZI,WAKUNGA
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya Ziada Sellah, akizungumzia maendeleo ya fani hiyo anasema, miaka ya nyuma wauguzi walikuwa wakiishia kupata mafunzo ngazi ya cheti na stashahada.
“Walikuwa hawapati mafunzo zaidi, baada ya kuona dunia inakimbia kwa kasi, tukaona na sisi Tanzania tunatakiwa kwenda kasi ndipo ikaanzishwa mafunzo ngazi ya shahada na wauguzi wengi wakaanza kufikia ngazi hiyo.
Tulianza kufika mbali zaidi na wauguzi na wakunga wakawa wanapata elimu ngazi ya uzamili
Hadi sasa ukiangalia tuna wauguzi wengi ambao wana shahada ya uzamivu, ambao wana uwezo wa kuchapisha maandiko,”anasema.
Ziada anasema katika fani ya uuguzi na ukunga wapo waliobobea.
Kwa upande wa changamoto Ziada anasema, vyuo vimekuwa vikiongezeka bila kuwa na udhibiti hali inayochangia wauguzi wanaohitimu kukosa ubora.
“Vikidhibitiwa unajua kabisa muuguzi au mkunga anayemaliza mafunzo anasifa zinazostahili kuwa katika fani hiyo.
Tunaamini tukikaa chini na kukabaliana na utitiri wa vyuo tutapunguza idadi ya wauguzi wasio na sifa na kuzalisha wenye ujuzi na stadi,”anasema.
Ziada anataja changamoto nyingine kuwa ni malamiko katika jamii yanayotokana na wauguzi na wakunga kukosa maadili.
Anasema, TNMC ina ukosefu wa fedha hivyo baraza lililozinduliwa linajukumu la kuhakikisha TNMC inapata rasilimali fedha, kutekeleza majukumu yake mbalimbali.
“Wananchi inayoikabili baraza ni wananchi kutofahamu kazi ya muuguzi na mkunga,”anasema..
Akizungumzia ukaguzi wa matibabu Ziada anasema, utaisaidia TNMC kuangalia ukaguzi wa kimatibabu.
“Tunakwenda kuangalia mkunga kafanya nini na mwisho wa siku tunagundua changamoto iko wapi.
Kuna dawati tumelianzisha linaloangalia huduma ambayo inajali utu heshima na maadili ya ukunga na uguzi, kila mgojwa anayekuja anahitaji kutambulika na anatakiwa kupata huduma bila kuwagawa katika makundi,’’anasema.
Ziada anasema,TNMC itahakikisha maadili ya wauguzi hayaendi nje ya maadili.
“Ili uwe muuguzi au mkunga ni lazima uwe na maadili yanayokufanya ufanye kazi,’’anasema.
Katika udhibiti wa ugonjwa wa Corona, Ziada anasema siku zote wapo mstari wa mbele na ndio wa kwanza katika udhibiti wa ugonjwa huo.
“Muuguzi anakuhudumia saa 24 siku saba katika wiki, ukiingia hospitali unakutana na muuguzi wa kwanza, ukilazwa unakuwa na muuguzi ukiruhusiwa upo na muuguzi
Kuhusu janga la corona sisi tuna nafasi kubwa kuhakikisha tunampa huduma mgojwa kulingana na changamoto alizonazo, daktari atakuja kwa ajili ya ushauri na kukuandikia dawa.
Muuguzi ndiye atakaye kujali, ana nafasi ya kutoa elimu kwa jamii kwani ni kazi yake kubwa kwa hiyo hii ni nafasi yetu kubwa,’’anasema.
Miaka mitatu ya TNMC, miongoni mwa mambo ya kujivunia ni wauguzi na wakunga walio hitimu katika vyuo mbalimbali kuidhinishwa.
Wauguzi na wakunga 8,983 wamesajiliwa na kupewa leseni, huku vyuo vipya vya uuguzi na ukunga vitatu vikianzishwa na 25 vikipanda kutoa mafunzo kuanzia ngazi ya astashahada hadi stsshahada.
Vilevile kwa mujibu wa TNMC vituo binafsi vya uuguzi na ukunga vitano viliidhinishwa
Mbali na hayo TNMC imesimamia matumizi bora ya taasisi na kuwachukulia hatua watumishi wasiofuata maadili, ambapo jumla ya watuhumiwa saba walifuatiliwa na kutiwa hatiani.
Pia baraza limeboresha kanzidata, ambapo wauguzi na wakunga wanapata huduma kwa njia ya mtandao.
BARAZA LA UUGUZI,UKUNGA
Msajili wa Baraza la Uuguzi na Wakunga Agnes Mtawa, anasema baraza hilo lilianzishwa mwaka 1953, chini ya sheria ya usajili uuguzi na ukunga
“Sheria hiyo ikafanyiwa marekebisho mwaka 1997 na mwaka 2010, sasa baraza linafanya kazi chini ya sheria namba moja ya mwaka 2010, ambayo imefanyiwa maboresho na kuifanya taaluma hii ikuwe.
Baraza lilipata hadhi ya kuwa taasisi mwaka 2014 na tangu hapo limetekeleza miongozo ya watoa taaluma kutoa huduma za uuguzi na ukunga.
Tayari tumeshatengeneza muundo na mfumo wa usajili ambapo idadi ya waguzi na wakunga kwa sasa ni rahisi kufahamika, tumetengeneza miongozo inayolenga kuboresha huduma za uuguzi na wakunga.
Agnes anasema hadi sasa wauguzi na wakunga waliopo nchini ni 46,000 huku TNMC ikiwa na mkakati wa miaka mitano ambao ndio muongozo wa kutoa huduma za uuguzi na ukunga yenye kufanya baraza hilo kusonga mbele,’
“Baraza lipo kuhakikisha jamii inapata huduma bora kwa kutatua changamoto, wanachama na watoa huduma wafuate sheria,”anasema.
Ili kuboresha huduma ya uuguzi na ukunga, Isaya Jacob anasema kufanyike uchunguzi ili wauguzi na wakunga wasio na sifa walio katika vituo vya afya waondolewe.